NA AHMED MAHMOUD, ARUSHA

WIZARA ya Maji, imeeleza itaendelea kushirikisha jamii katika ulinzi wa mito na vyanzo vingine vya maji, ili visivamiwe, visiharibiwe na kuchafuliwa mazingira yake badala yake vitunzwe na viendelee kuwepokwa ajili ya vizazi vijavyo.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa usimamizi wa rasilimali za maji katika wizara ya maji, Rosemary Rwebugisa alipokuwa akizindua Jukwaa la Watumiaji kidakio cha maji cha mto Themi, jijini Arusha kinachosimamiwa na taasisi ya bonde la mto Pangani kwa ajili ya kusimamia matumizi ya maji ya juu na chini ya ardhi ili yaendelee kuwepo kwa wakati wote wa kiangazi na masika.

Alisema lengo la wizara ni kulinda, kusimamia utunzaji na usambazaji wa maji kwenye mabonde yote tisa ya maji likiwemo bonde la Pangani na mto Ruvu, lengo ni kuhakikisha yanakuwepo matumizi sahihi ya maji kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo mito na hivyo kukomeshwa na kudhibitiwa kwa uvamizi na uchafuzi wa vyanzo hivyp ili yawepo matumizi endelevu.

Alisema jukumu la Jukwaa hilo ni kufahamu changamoto ziliyopo na kushiriki katika utatuzi wake na kuwa walinzi wa mito hiyo sanjari na kuibua changamoto ambazo zitasaidia kuondoa changamoto ya uharibifu wa mazingira na ukosefu wa maji.

Rwebugisa, alisema hali ya upatikanaji wa maji nchini inaridhisha, msisitizo ni kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa na kutunzwa kwa ajili ya viazi vijavyo, na kuzingatia nchi yenu imefikia uchumi wa kati.

Alisema uchafuzi wa mazingira unatokana na shughuli za kibinadamu zikiwemo kilimo kandokando ya mito, utupajitaka mitoni, ujenzi nyumba kandokando ya mito, shughuli za kilimo,utiririshaji wa majitaka mitoni,kuoshea magari mitoni.

Nae Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini, mkoa wa Arusha (RUWASA) Joseph Makaidi, alisema taasisi hiyo imeanzishwa mwaka 2019 kwa ajili ya kupanga, kuratibu na kusanifu shughuli za maji Vijijini licha ya kuwepo uharibifu wa mito na vyanzo vingine unatokana na matumizi ya rasilimali ya maji.

Nae Mkurugenzi wa bonde la mto Pangani, Segulesegule, alisema bonde hilo linahudumia mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro na. wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, ambayo mito iliyopo hutiririsha maji Bahrain ya Hindi.

Alisema licha ya kuwepo sheria anahimiza kwanza itolewe Elimu kwa umma ili jamii iwe ni walinzi wa mito na vyanzo vyake pamoja na utunzaji mazingira ili kutokuchafua maji kutokana na shughuli za kibinadam, ikiwemo utupaji taka, utiririshaji ,majitaka, kulima kandokando ya mito kulisha Mifumo, kujenga makazi ya kudumu, kuoshea magari mitoni.