KINSHASA,DRC
WATU 12 wameuawa Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kushambuliwa na waasi katika mji wa Mwenda mkoani Kivu Kaskazini na Murubia huko Ituri.
Taarifa zinasema hujuma hiyo ilitekelezwa na waasi wa ADF ambao asili yao ni Uganda lakini wana ngome yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Usalama unaendelea kuzorota katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri.
Wakaazi wa eneo la Mwenda, Wilayani Beni walilazimika kuyahama makaazi yao, baada ya kuripotiwa visa mbalimbali vya mashambulizi.
Na katika mkoa wa Ituri hali ya usalama imeendelea kudorora.
Akihojiwa na waandishi habari,Wilson Mugara,mmoja wa madiwani waliochaguliwa katika maeneo ya Murubia alisema kuwa watu 7 wameuawa na Ng’ombe 200 waliibwa na waasi, taaarifa ambayo bado inachunguzwa.
Serkali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inayashtumu makundi ya ADF na Codeco kuendelea kuhatarisha usalama katika mikoa ya mashariki mwa DRC.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza operesheni mpya ya kupambana na waasi wa ADF tarehe 30 Oktoba mwaka jana 2019.