NA MWAJUMA JUMA

WACHEZAJI wa timu ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) wametakiwa kufuata utaratibu wa adhabu waliojiwekea ili kutunza nidhamu ndani ya timu hiyo.

Wito huo umetolewa na Katibu wa timu hiyo  Mohammed  Haji Nassor “kipamba” alipokuwa akizungumza na wachezaji hao mara baada ya kumaliza mazoezi kwenye uwanja wa Nyuki Maisara.

Alisema wakati uongozi wametoa utaratibu huo na kukubalika na wote si jambo zuri  kuona wengine wanaufuata na waliobakia wanadharau.

Alifahamisha kwamba kufanya hivyo kunapunguza nidhamu ya timu na kuiweka katika hali ambayo sio nzuri katika michezo.

Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo Khalfan Simai alisema utaratibu waliojiwekea sio  adhabu bali ni jumla ya mazoezi.

Timu hiyo imejiwekea utaratibu wa mchezaji ambae atachelewa kufika katika mazoezi azunguruke uwanja mara tatu na kwa ambae hakwenda kwenye mechi pasipo na kutoa taarifa siku anayokuja kwenye mazoezi atatakiwa azunguruke uwanja mara tano.