NA TATU MAKAME
KAMISHENI ya utalii Zanzibar imesema umefika wakati kwa wadau wa sekta hiyo kutafuta masoko ya ndani badala ya kutegemea ya nje pekee hasa yanapojitokeza majanga ya dharura ikiwemo janga la corona.
Katibu Mtendaji Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk. Abdalla Mohamed Juma, alisema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunguliwa kwa kongamano la siku mbili la wadau wa utalii linaloendelea katika Hoteli ya Verde iliyopo Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Alisema ingawa utalii umerudi katika visiwa vya Unguja na Pemba, lakini mbinu mpya za kutafuta masoko ya ndani zinahitajika ili kuziba pengo lililojitokeza wakati dunia ilipokumbwa na janga la ugonjwa huo kulikopelekea watali kutikuja nchini.
Hata hivyo, alisema kufanyika kwa kongamano la wadau wa utalii kutafungua milango ya kupata mbinu za kutafuta masoko mapya kupitia sekta hiyo na kutoa changamoto zao ili zifanyiwa kazi.
Dk. Juma, alieleza kuwa hivi sasa Kamisheni imejipanga upya kuangalia athari iliyojitokeza katika kipindi chote cha ugonjwa huo hivyo aliwataka wadau kutumia muda huo kutoa maoni yao.
“umefika wakati tubadilishe mtazamo wetu kuangalia utalii wa ndani kutumia wadau wetu wa ndani badala ya kutegemea wageni hasa katika kipindi kama hichi”,alisema.