BAMAKO,MALI

VIONGOZI wa mapinduzi ya kijeshi  Mali wameuambia ujumbe wa wapatanishi wa Magharibi mwa Afrika kuwa wanataka kubakia madarakani kwa miaka mitatu ya kipindi cha mpito.

Wapatanishi kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas) walitumwa Mali mwishoni mwa wiki kufanya majadiliano na maofisa jeshi wa Mali waliompindua Rais Ibrahim Boubacar Keita tarehe 18 mwezi huu ili kuurejesha utawala wa kiraia nchini humo.  

Hata hivyo siku tatu za mazungumzo hayo zimekwisha bila ya kufikiwa uamuzi kuhusu muundo wa Serikali ya mpito.

Kiongozi aliyewaongoza wanajeshi katika mapinduzi huko Mali alisema baada ya kunyakua madaraka kwamba,wamechukua hatua hiyo kwa sababu nchi ilikuwa inatumbukia katika hali ya machafuko na ukosefu wa usalama.

Ofisi ya Rais wa Nigeria ilisema kuwa, Goodluck Jonathan Mpatanishi wa jumuiya ya Ecowas alisema kuwa wafanya mapinduzi nchini Mali wanataka kuongoza kipindi cha mpito nchini humo kwa muda wa miaka mitatu kabla ya uchaguzi.

Hata hivyo mpatanishi huyo alisema kuwa, waliwaeleza wafanya mapinduzi hao wa Mali kwamba, jumuiya ya Ecowas itakubali Serikali ya mpito chini ya uongozi wa kiraia au iongozwe na ofisa jeshi mstaafu, ambayo itapasa idumu kwa muda wa miezi sita au tisa, na  kama ni zaidi, basi iweko madarakani kwa muda wa miezi 12.