NA HUSNA SHEHA

JUMLA ya wafanyabiashara 957 wa aina mbalimbali za vyakula, wamekamatwa na Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’ kwa kushindwa kutii sheria za uuzaji wa vyakula kwa kipindi cha Januari hadi Agosti 20 mwaka huu.

Wafanyabiashara hao walikamatwa kutokana na kushindwa kufuata masharti waliyopewa na Manispaa hiyo ikiwemo kuvaa sare, kupima afya, kuuza bidhaa zilizomaliza muda,na kutofanya usafi katika  maeneo ya biashara .

Mkuu wa Huduma za Jamii wa Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’ Asha Salum Bakari, alisema hayo Ofisini kwake Kianga Mkoa wa Mjini Magharibi , wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema zoezi hilo lilifanywa kuwepo kwa wafanyabiashara ambao wanaendesha shuhuli zao kinyume na masharti waliyopewa na manispaa.

Alifahamisha kuwa katika zoezi hilo wafanyabiashara 300 walipewa adhabu ya papo kwa papo ya kulipa faini ya shilingi 50,000, kwa kila mmoja na 20 kati yao walifikishwa mahakamani na walipewaadhabu ya kulipa faini ya shilingi 300,000 kila mmoja.

Hata hivyo, alisema wafanyabiashara wadogo wadogo walipewa elimu juu ya kufuata masharti ya afya na zoezi la ukaguzi kwa wafanyabiashara  litaendelea ili lengo la kuwabaini wanaouza biashara kinyume na taratibu na vigezo vilivyotolewa na Wizara ya Afya.