Wataka mashahidi wakamatwe wanaokataa kufika Mahakamani

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WANAFUNZI wa Chuo cha Mafunzo Wete, wameiomba Mahakama Kuu Zanzibar, kujibiwa rufaa zao kwa wale walioomba, kwani zinacheleweshwa sana, jambo ambalo linawasababishia wengine kumaliza kutumikia chuo hicho bado hawajazipata.

Wakizungumza mbele ya Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, wanafunzi hao walieleza kuwa, ni muda sasa wameomba rufaa bila ya kujibiwa na wala hawapati jibu muafaka juu ya ucheleweshaji huo.

Walisema kuwa, rufaa wanazoomba zimekuwa zikicheleweshwa kiasi kwamba wengine humaliza muda wao bila kupata na kumuomba Jaji huyo kufuatilia rufaa zao ili wawe na amani.

“Kwa kweli tunakata tamaa, tumeomba rufaa, majibu hatupati na ni muda mrefu sasa, chakusikitisha wengine wanafikia kumaliza muda wao rufaa hawajapata, hii inauma”, walisema wanafunzi hao.

Aidha walieleza kuwa, kuongezewa miaka kwa mshtakiwa baada ya kukata rufaa kunawatia hofu na kuwasababishia wenye nia ya kuomba kusitisha.

“Tunaona kesi nyingi hapa hasa za udhalilishaji, ukikata rufaa tu unazidishiwa miaka, hivyo tunapata hofu ya kuomba”, walisema wanafunzi hao.

Kwa upande wa watuhumiwa waliopo rumande walimuomba Jaji Mkuu, kuwekwa Jaji mkaazi kisiwani Pemba, ili kesi zao zimalize kwa haraka na kuepuka usumbufu.

“Kila tukienda mahakamani shauri linapangwa tarehe nyengine, hivi tunachoka maana makosa mengine hayana dhamana, kwa hiyo tunakumba utuletee Jaji mkaazi kisiwani Pemba”, walisema.