NA LAILA KEIS

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa hatua ya kwanza imewapitisha wagombea ubunge 53 na kuwaondoa 10 baada ya kukosa vigezo kuingia katika kinyanganyiro hicho, huku mmoja wa Chama cha ACT Wazalendo aliyewekewa pingamizi imepanguliwa baada ya kushinda.

Msimamizi msaidizi ngazi ya jimbo, wilaya ya Mjini, Aisha Mahboub Juma, alieleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili huko Ofisi za Tume Maisara mjini Unguja, baada ya kumalizika zoezi la urejeshaji fomu za kuwania nafasi hiyo na kuruhusu kuanza kwa zoezi la kupiga kampeni.

Akifafanua juu ya zoezi hilo alisema kwa wilaya hiyo, wagombea waliochukua fomu kutoka kwenye vyama 19 tofauti vilivyosajiliwa mwaka huu walikuwa ni 67, ambao waliorejesha ni 62.

Aidha alisema, kati ya 62 waliorejesha fomu, wagombea 10 hawakutimiza masharti yaliyowekwa kisheria, ambao hawatoruhusiwa kuendelea na zoezi la kugombea na mgombea mmoja kutoka chama cha ACT, Mohamed Yussuf Maalim, Jimbo la Jang’ombe, hapo awali aliwekewa pingamizi, lakini alishinda na kuidhinishwa kuwa mgombea.

Naye msimamizi msaidizi ngazi ya jimbo wilaya ya Magharibi ‘B’, Abuubakar Hassan Chumu, alisema, kwa majimbo matano ya wilaya hiyo, ni wangombea 48 waliochukua fomu kutoka vyama 14, ambao waliorejesha ni 39, kati yao walioteuliwa ni wagombea 37.

Akifafanua kuhusu suala la pingamizi kwa wagombea, msimamizi msaidizi ngazi ya jimbo wilaya ya mjini, Ramadhan Abdallah Bakari alisema, wagombea walioteuliwa kwa sasa, wasijiachie na kusahau kuwa bado kuna kipengele cha pingamizi kutoka vyama vya siasa.

“Wagombea watatakiwa waonyeshe fomu za gharama watakazozitumia kwenye zoezi zima la uchaguzi, vyanzo vyao vya fedha na kima watakachokitumia, ikiwa wataenda kinyume na walivyoahidi, msajili wa vyama vya siasa atatoa pingamizi kwa mgombea huyo” alifafanua.

Vile vile, aliwataka wateule wote, kufanya kampeni kwa amani na utulivu, bila kuleta vurugu na machafuko katika jamii.