NA MADINA ISSA
WAGOMBEA wa Ubunge wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya ya Mjini, wameridhika na zoezi la uchukuaji fomu na urejeshaji uliofanywa na Tume ya Tiafa ya Uchaguzi kwa upande wa Zanzibar.
Wagombea hao waliyaeleza hayo kwa nyakati tofauti, baada ya zoezi hilo kumalizika katika Ofisi ya Wilaya ambapo walisema wamepata ushirikiano mkubwa ndani ya Tume hiyo.
Wagombea hao ni Injinia Hamadi Yussuf Masauni anayegombea Jimbo la Kikwajuni, Ali Hassan Omar (Kingi) Jimbo la Jang’ombe, Ahmada Yahya Abdul-wakil jimbo la Kwahani na Mohamed Suleiman Omar Jimbo la Malindi.
Injiania Masauni alisema, zoezi la upatikanaji wa wadhamini katika zoezi hilo, limekwenda vizuri na kuahidi kuwatumikia wananchi wa Kikwajuni kwani wameonesha mwanga na mapenzi ya kumuamini katika utendaji wa kazi zake.
“Mimi Ubunge wa jimbo hili, sikuanza leo hivi ni kipindi changu cha tatu kugombea jimbo hili, hivyo, imani yangu kufanya mazuri niliyoyafanya kwa jimbo langu” alisema.
Aidha Masauni, alisema kuwa katika ujazaji wa Fomu hiyo, alikutana na changamoto ya wananchi wanaotaka kumdhamini katika fomu hizo, kutokana na sheria za tume zilizoweka hawakuweza na amewaahidi atawatumikia kwa nguvu zake kwa kuwapelekea maendeleo wananchi wa jimbo hilo.
Mgombea wa jimbo la Jang’ombe Ali Hassan Omar (Kingi), alisema kuwa katika kuwapata udhamini hakupata shida na wananchi walijitokeza kwa wingi katika kumdhamini na aliwaahidi wananchi kuwapelekea maendeleo endapo wakimpitisha tena kuwa Mbunge wa jimbo hilo.