NA HAFSA GOLO

ZOEZI la Uchukuaji fomu wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja linaendelea kwa kasi ambapo vyama vya siasa 14 vimejitokeza huku wachukuaji fomu hadi saa 4:15    asubuhi Agasti 22 walifikia 37.

Aidha kati ya watu 37 waliochukua fomu nafasi ya ubunge kupitia vyama mbali mbali vya siasa 16 walikuwa ni wanawake.

Alieleza hayo Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Said Khamis Ramadhan kwa niaba ya Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Wilaya ya Magharibi ‘A’, Hidaya Mrisho Ali katika ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyopo Mwera Unguja.

Alisema kwa mujibu wa vyama vya siasa 19 vilivyosajiliwa Tanzania mwaka 2020 nusu na robo ya vyama hivyo tayari vimeitikia wito wa uchukuaji fomu.

Aidha alisema hatua hiyo imedhihirisha kukuwa kwa demokrasi nchini Tanzania sambamba na wananchi kutumia haki yao ya msingi ya kuwania nafasi za uongozi bila ya kujali itikadi wala jinsia.

Hata hivyo alisema anaamini kutokana na kuwepo kwa muda upo uwezekano kwa vyama vyengine vilivyosalia vitatumia nafasi hiyo kwa kuwasilisha wagombea wao.

Alitumia muda huo kuwataka watu wote waliojitokeza kuchukua fomu hizo wajaze na kuzirudisha kwa wakati ili kuepuka pingamizi.

Mmoja kati ya wagombea, waliojitokeza katika uchukuaji wa fomu hizo kupitia CCM, Maulid Salum Ali alisema, Tanzania ni nchi inayoendelea kuimarika kwa demokrasia sambamba na kukua kwa haki na fursa sawa kwa wananchi.

Alisema kustawi kwa hali hiyo imechangia kuleta hamasa na muitikio kwa wananchi kuwania nafasi za uongozi.