TRIPOLI, LIBYA
UMOJA wa Mataifa umesema takribani wahamiaji 45 walifariki wiki hii baada ya meli yao kuzama katika pwani ya Libya.
Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na wakimbizi na wahamiaji,yalisema katika taarifa yake kwamba miongoni mwa waliofariki wamo watoto watano na kuitaja ajali hiyo ya kuzama meli kuwa ndio kubwa ndani ya mwaka huu.
Wahamiaji wengine 37 wengi kutoka Senegal, Mali, Chad na Ghana, waliokolewa na wavuvi na baadae kukamatwa baada ya kurejeshwa Libya.
Mashirika yote mawili yalizitaka nchi kubadili mkakati wa kulishughulikia suala hilo katika bahari ya Mediterenia na Libya, ambayo imekuwa njia ya wahamiaji wanaojaribu kuzikimbia nchi zao wakitaka kuingia Ulaya.
Hadi sasa takrribani wahamiaji na wakimbizi 302 walipoteza maisha baharini ndani ya mwaka huu.