KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi amefungua kikao kazi cha Maafisa wanadhimu na wahasibu kutoka makao makuu ya Polisi, Mikoa na Vikosi Tanzania Bara na Visiwani.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kinachofanyika katika ukumbi wa Shule ya Polisi Tanzania – Moshi (CCP), kikiwa na kaulimbiu inayosema “UADILIFU KATIKA USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA HUCHAGIZA MAENDELEO “

Akifungua kikao hicho Katibu huyo, amewataka washiriki kushiriki kikamilifu katika kujadili changamoto zilizopo katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuzipatia ufumbuzi.

Aidha amewataka kila mmoja kwa nafasi yake kuacha alama kwa kuleta mabadiliko chanya katika eneo lake la kazi, ili serikali iweze kunufaika na uwepo wake.

Pia amesisitiza swala la kuwa na weledi na uadilifu wa hali ya juu, uwajibikaji, Usiri na kuweka mazingira mazuri ya kila mmoja kuwa muadilifu katika kusimamia mali za umma.

Amewapongeza washiriki na Jeshi la Polisi kwa ujumla kwa kufanikiwa kuwatumia wataalamu wake wa ndani na kufanikiwa kutengeneza mfumo wa ukusanyaji wa maduhuri ya serikali.

Kaimu Kamishina wa Fedha na Lojistiki, Naibu Kamishina Kidavashari ambaye alimwakilisha Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania katika kikao hicho, alisema washiriki wamejadili changamoto zilizopo katika usimamizi wa rasilimali fedha ndani ya Jeshi la Polisi.