MKOA KUSINI
WAZAZI na walezi wametakiwa kutoa mashirikiano kwa walimu pamoja na kamati za skuli, ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu kwa ufanisi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud katika hafla ya kuwakabizi zawadi wanafunzi waliofaulu kidato cha pili katika skuli ya Ghana iliyopo wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema endapo wazazi na walezi watashirikiana na walimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi hao watafanikisha kwa kiasi kikubwa malengo ya walimu ya kuleta ufaulu mzuri kwa wanafunzi.
Aidhaa Ayoub amesema kamati ya maendeleo ya elimu ya shehia ya Ghana imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha inaanza ujenzi wa madarasa mengine mapya, ili kusudi kuhamasisha wengine kuchangia ujenzi wa madarasa hayo ambapo amewataka wananchi kuchangia katika miradi ya
kijamii ikiwemo ujenzi wa madarasa katika skuli hiyo.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Elimu ya shehia ya Ghana, Ali Mohammed Othman, amesema kamati imefikia katika mafanikio mazuri ikiwemo kuifanya jamii kuwa na muamko juu ya masuala ya elimu, kuongeza ufaulu wa wanafunzi, kuweka kambi za wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani ya taifa pamoja na kuanzisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Nae mfanyabiashara Said Nassir Bopar, amesema katika hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua sekta ya elimu ameahidi kuisaidia skuli hiyo mabati 150 ya kuezekea sambamba na kompyuta tano zitakazo ongeza ufanisi kwa wanafunzi wa skuli hiyo.
Vifaa vilivyokabidhiwa kwa ni pamoja na laptot , mikoba pamoja na vifaa vya kusomea , ambapo Jumla ya asilimia 79.29 ya wanafunzi wote wa kidato cha pili wa skuli hiyo walifanikiwa kujiunga na kidato cha tatu huku skuli hiyo ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba na uchakavu wa majengo, pamoja na kukosekana kwa hati miliki ya skuli hiyo.