LONDON,UINGEREZA

SERIKALI ya Uingereza imesema wasafiri kutoka nchini humo kuelekea Ufaransa wanapaswa kujiweka karantini ili kuhakikisha hawana dalili za virusi vya corona au kwamba wamekaribiana na mtu aliyethibitishwa kuwa na virusi hivyo ndani ya siku 14 kabla ya safari zao.

Serikali hiyo ilisema pia wasafiri watakaokuwa wanarejea nchini kutoka Ufaransa baada ya Agosti 15 watapaswa kujiweka karantini kufuatia viwango vya juu vya maambukizi nchini Ufaransa.

Masharti haya yamewekwa baada ya kuathiri maeneo Waingereza wanayopenda kutembelea wakati huu wa msimu wa kiangazi huku mashirika ya ndege yakipambana kubakia katika biashara.

Mataifa mengine yakiwemo Uhispania, Uholanzi, Ubelgiji, Croatia na Austria tayari yapo katika orodha ya Serikali ya wasafiri wanaopaswa kuwa karantini.

Mapema mwaka huu Uingereza ilikosolewa kuchelewa kuchukua hatua ya kuweka masharti ya kuwataka watu kubakia majumbani mwao mwanzoni mwa janga la corona hali iliyosababisha visa vingi vya maambukizi nchini humo.