NA MARYAM HASSAN
JUMLA ya wakulima 22 wa zao la mpunga Zanzibar wamepelekwa Morogoro kwa lengo la kujifunza zaidi mbinu bora za uzalishaji wa zao hilo.
Wakulima hao wakiwa pamoja na Mtaalam wa mbegu bora kupitia mradi wa ERPP Mohammed Faida Haji, na kueleza ziara hiyo ya siku nne ikiwa ni muendelezo wa kuwapatia mafunzo wakulima hao.
Akizungumza na Zanzibar Leo mtaalamu huyo, alisema wakulima hao ni wale ambao mabonde yao yamepitishwa miundombinu ya kumwagilia maji katika mabonde manane kwa Unguja na Pemba.
Pia alisema kuwa wakulima hao watabadilishana mawazo kwa kupeana mbinu bora baina ya wakulima wa Zanzibar na Tanzania bara, kwani katika ziara hiyo imejumuisha mabwana shamaba wanane ,ambao nao watapatiwa mbinu za kuwasaidia wakulima.
Mabonde hayo kwa upande wa Unguja ni Kibonde Mzungu, Mchangani, Koani na Bandamaji huku Pemba ni Kwale mpoma, Ole, Dobi na Machigini.
Nae bibi shamba, Aviwe Juma Nassor, kutoka Mchangani alisema ziara hiyo itawasadia kujifunza mbinu mbali mbali za kuzalisha mpunga licha ya kupewa mafunzo na wataalam wa kilimo kisiwani Zanzibar.