NA LAYLAT KHALFAN
WALIMU Wakuu wa Wilaya ya Mjini, wametakiwa kuwasimamia vizuri walimu wao katika kuendeleza elimu kwa wanafunzi ili ubora wa elimu uweze kufikiwa.
Mkurugenzi Baraza la Manispaa Mjini, Said Juma Ahmada, aliyasema hayo katika ukumbi wa Baraza hilo, alipokuwa akiwanasihi walimu wakuu kutoka skuli mbalimbali za manispaa hiyo katika kuimarisha utendaji ndani ya skuli hizo kikao ambacho kulifanyika Malindi Mjini Zanzibar.
Alisema taifa linapokuwa na elimu maendeleo yanakuwa kwa haraka, hivyo walimu wakuu wana nafasi kubwa ya kusimamia walimu waliopo sehemu husika sambamba na kuleta ushindani wa kupasisha wanafunzi.
“Walimu wakuu mna haki ya kusimamia nidhamu ambazo zinaoneshwa na wanafunzi hii itasaidia kuimarisha ufaulu bora wa wanafunzi,”alisema.
Aidha, Said alifahamisha kuwa, wakati umefika sasa kuona walimu hao wanatumia uwezo wao na mbinu zao katika kukamilisha silabas, ili wanafunzi wafanye vizuri katika masomo yao na mitihani yao kwa ujumla.
“Silabas iliyopangwa hakikisha mwalimu unamaliza thubutu kufuatilia achana na mazoea ya kukaa ofisini hii itamjenga mwalimu kuwa makini na kazi yake”, alisema.
Alisema iwapo mwalimu mkuu atakuwa hufuatilii kazi za walimu wake katika ufundishaji watoto wengi watafeli na kupoteza ndoto zao walizojiwekea, huku ukizingatia taifa linawategemea zaidi vijana hao.
Alieleza kuwa, mfumo wa ugatuzi ukiutathmini umekuwa na tija na mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, Afya na kilimo, hivyo iwapo msimamizi atakuwa makini kuwajibika, ufaulu bora wa kiwango cha upatikanaji wa elimu utaimarika.
Akigusia utoro katika skuli, Said alisema ni jambo la kuskitisha kuona wanafunzi hawahudhurii skuli ipasavyo, hivyo aliwatahadharisha walimu hao kusimamia suala hilo na kulichukulia hatua kwa mujibu wa miongozo ya elimu.
Naye Ofisa Elimu wa Baraza hilo, Ali Omar Ali, alisema nchi inahitaji maendeleo hivyo ni lazima elimu inayotolewa kwa vijana hao iwe na kiwango kinachokubalika kwa lengo la kupata viongozi makini wa baadae.
Nao walimu hao walimshukuru Mkurugenzi huo, na kuahidi kuyafanyia kazi yale yote walioamrishwa ili ufaulu kwa wanafunzi uzidi kukua siku hadi siku.