NA HAJI NASSOR, PEMBA

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar ‘BMEJZ’ imesema uwepo wake na kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanafunzi nchini, ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar kuwapatia elimu bure wananchi wake.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mratibu wa Bodi hiyo kisiwani Pemba Ahmada Omar Juma, wakati alipokua akizugumza na wanafunzi na wahitimu wa kidato cha sita ukumbi wa skuli ya sekondari ya Madungu Chake Chake.

Alisema, baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, serikali ilitangaaza elimu bure, na kisha kuwepo kwa michango ingawa kwenye awamu ya saba ya uongozi wa Rais wa Zanzibar chini ya Dk: Ali Mohamed Shein, imefuta michango hiyo.

Alisema michango hiyo ilifutwa kuanzia ile ya elimu ya msingi na sekondari, na kisha mwaka 2011, ilipitishwa sheria ya kuanzisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, yenye wajibu wa kutoa mikopo kwa wazanzibari wenye sifa za kuendelea na elimu ya juu.

Mratibu huyo alieleza kuwa, uwepo wa bodi hiyo na kutoa mikopo isiyo na riba ni dhamira njema ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuhakikisha, wazanzibar hawana sababu ya kukosa kujiendeleza elimu ya juu.

Hivyo Mratibu huyo amewataka wananchi wa Zanzibar wenye sifa, kuchangamkia fursa hiyo, ambayo katika baadhi ya nchi hakuna aina ya bodi hiyo.

Aidha Mratibu huyo, alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wale wanaodaiwa na bodi ya Mikopo kurejesha fedha hizo, ili na wengine wapate kuziomba na kujisomea huku wakielewa kwamba haziko kwa ajili ya kufanyia anasa.

Mapema Kamishan wa watendakazi kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, Salama Ramadhan Makame, amewamekumbusha wananfunzi nchini kuwa, mkopo wa fedha kwa ajili ya elimu ya juu, unaotolewa na Bodi ya mikopo, hapewi kila muombaji, bali lazima kuzingatiwe kwa vipaumbele vya nchi, ili watakaohitimu waweze kukubalika kwenye soko la ajira.

Alisema, serikali baada ya kufanya utafiti na kujiridhisha, iligundua kuwa, ilikuwa ikisomesha wataalamu wa fani moja pekee, ingawa baadaa ya kugundua hilo, sasa imeamua kuangali soko la ajira lilivyo.

Alisema kuwa hapo awali, kulikuwa na makundi makubwa yalioko mitaani ya wanasheria na wahasibu, wakati serikali ikihitaji wataalamu wengine mbali mbali kama vile wa mafuta na gesi.

Kamishna huyo alieleza kuwa, ndio maana kila mmoja ana haki ya kuomba mkopo kwa ajili ya elimu ya juu, lakini sio kila muombaji anaweza kupewa, kutokana na serikali kuweka vipaumbele vyake.

Mapema Afisa Habari wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar ‘BMEJZ’ Khamis Haji Omar, alisema miongoni mwa nyaraka husika zinazotakiwa kwa kila muombaji wa mkopo, ni kitambulisho cha mzanzibari mkaazi na  awe na cheti cha kumalizia masomo ya kidato cha nne au sita, wadhamini wawili sambamba na kuzingatia vipaumbele vya nchi ambavyo vimeteuliwa.