WANAJESHI walioongoza mapinduzi dhidi ya rais wa taifa hilo Ibrahim Boubacar Keita aliyelazimisha kujiuzulu wameripotiwa kutangaza kwamba wataiongoza serikali ya mpito na kuandaa uchaguzi mpya.

Wanajeshi hao walianzisha uasi hapo juzi, katika mji wa Kati na baadae kuelekea mji mkuu Bamako, umbali wa kilomita 15 na kwenda kumlazimisha rais wa nchi hiyo ajiuzulu.

Kanali-meja Ismael Wague ambaye ni mkuu wa utumishi wa jeshi la Mali ametangaza kupitia kituo cha televisheni cha taifa kuundwa kwa kamati ya kitaifa ya uongozi nchi.

Alisema, mapinduzi ya kijeshi yalikuwa ni ya lazima kwa kuwa serikali ya Keita iliitumbukiza Mali kwenye machafuko na kukosekana kwa usalama.

Tamko hilo limekuja saa chache baada ya Keita kutangaza kujiuzulu katika hotuba ya moja kwa moja iliyorushwa kupitia televisheni, baada ya mapinduzi hayo yaliyoshuhudia wanajeshi wakiwakamata Keita na waziri mkuu wake Boubou Cisse.

Wague alisema”Mvutano wa kijamii na kisiasa umedidimiza utendaji wa nchi kwa muda mrefu na maandamano yamekuwa yakifanyika tangu uchaguzi uliopita yanathibitisha kuwa nchi haiko sawa.

“Mali ni nchi kubwa, tajiri na tamaduni zake tofauti, tajiri kwa ardhi yake, utajiri wa watu wake, tajiri wa wanyama na mimea, lakini ambaye uwepo wake kama nchi na taifa unatishiwa katika misingi yake yote ya uasisi”, alisema.

Taarifa ya kujiuzulu Keita ilipokelewa kwa shangwe na waandamaji wanaoipinga serikali katika mji mkuu, Bamako lakini ikipokelewa kwa tahadhari na Ufaransa ambayo Mali iliwahi kuwa koloni lake pamoja na washirika wengine na mataifa ya kigeni.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana baadae leo kujadili hali inavyoendelea nchini Mali ambako Umoja wa Mataifa una wanajeshi 15,600 wanaolinda amani.

Keita aliyechaguliwa kidemokrasia mwaka 2013 kwa ushindi wa kishindo na kuchaguliwa tena miaka mitano baadae, bado alikuwa na miaka mitatu ya kuhitimisha awamu yake.

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS iliwahi kupeleka wasuluhishi kujaribisha makubaliano ya serikali ya kitaifa, ingawa mazungumzo hayo yalishindikana, baada ya kudhihirika kwamba waandamanaji wasingekubali chochote zaidi ya Keita kujiuzulu.

Kwenye tangazo lake la kujiuzulu, Keita alisema hangependelea kuona damu inamwagika na hivyo ameamua kuachia ngazi. Aidha, alitangaza kuivunja serikali yake na bunge la kitaifa.

Anguko la kisiasa la Keita, linashabihiana kwa karibu na lile la mtangulizi wake, Amadou Toumani Toure aliondolewa kwa nguvu kwenye wadhifa huo mwaka 2012.

Mapinduzi ya kijeshi Mali, je ni kina nani waliopanga na kutekeleza?

Wahusika wa mapinduzi ya Mali yaliomuondoa rais wa taifa hilo Ibrahim Keita ni pamoja na naibu kiongozi wa kambi za kijeshi na jenerali aliepata mafunzo yake nchini Ufaransa.

Ibrahim Boubacar Keita

1. Kanali Malick Diaw: Ni naibu kiongozi wa kambi ya jeshi ya kati ambapo mapinduzi hayo yalianzia. Kuna habari chache kumuhusu mbali na ripoti kwamba alitoka katika mafunzo ya kijeshi nchini Urusi.

Alisimama kandakando ya naibu ofisa mkuu wa jeshi kanali Ismale Wague ambaye alisoma taarifa kwa niaba ya vuguvugu la Junta ili kutangaza mapinduzi hayo ya kijeshi.

Kanali Diaw anaaminika kuwa kiongozi wa mapinduzi katika kambi hiyo ya Kati, kilomita 15 kutoka Bamakoi. Anadaiwa kumuomba rais kuondoka madarakani kabla ya saa nane mchana, ujumbe wa twitter ulisema kumuhusu.

2. Kanali Sadio Camara:  Kanali Camara ni mkurugenzi wa zamani wa chuo cha mafunzo ya kijeshi. Tovuti ya Mali iliripoti kwamba alizaliwa 1979 katika eneo la Kati, katika jimbo la Kusini la Koulikoro. Alifuzu kutoka chuo cha kijeshi cha Koulikoro.

Baadaye alipelekwa katika eneo la kaskazini mwa Mali ambapo alihudumu chini ya jenerali El Hadj Gamou hadi 2012. Kanali Camara baadaye alikuwa mkurugenzi wa chuo cha mafunzo ya kijeshi cha Kati, nafasi alioshikilia hadi Januari 2020 wakati alipoelekea Urusi kwa mafunzo ya kijeshi.

Gazeti la Mali Tribune lilisema kwamba alirudi Bamako mapema mwezi huu kwa likizo yake mwezi mmoja. Kanali Camara alipendwa na kila mtu ambapo alifanya kazi na anaheshimiwa na wadogo zake wote.

3. Jenerali Cheick Fanta Mady Dembele: Jenerali huyo  ni mkurugenzi wa taasisi ya kuweka amani ya Alioune Blondin Beye.

Alipandishwa cheo hadi kufikia cheo cha Brigedia jenerali na kuchukua uongozi wa taasisi hiyo ya kulinda amani mwezi Disemba mwaka 2018.

Kabla ya kupandishwa cheo katika taasisi hiyo, jenerali Dembele alikuwa akisimamia migogoro na mipango ya kimkakati katika tume ya amani na usalama barani Afrika ilio na makao yake makuu Addis Ababa, Ethiopia.

Jenerali Dembele alifuzu katika chuo kikuu cha kijeshi cha Saint-Cyr military nchini Ufaransa, pia alihitimu kutoka chuo cha General Staff College huko Koulikoro, Mali.

Anamiliki shahada ya historia kutoka chuo kikuu cha Paris cha I Panthéon-Sorbonne, pia anamiliki stashahada katika uhandisi na alifuzu kutoka chuo kikuu cha Federal Army University mjini Munich, Ujerumani.