KINSHASA,DRC
JESHI la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo limetangaza kuwa wanamgambo wa kundi la ADF wameuwa raia 20 katika hujuma dhidi ya vijiji vitatu mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa zinasema maofisa wa usalama walipata maiti za watu waliouawa Jumatano katika vijiji vya Mapasana,Mayitike na Sayuni, yapata kilomita 30 kaskazini magharibi mwa mji wa Beni.
Mauaji hayo yalifanyika siku tatu baada ya hujuma kama hiyo iliyopelekea watu 13 kupoteza maisha.
Waasi wa Uganda wa Allied Democratic Forces (ADF) wako mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu mwaka 1994 ambako wamekuwa wakifanya jinai na hujuma mbalimbali dhidi ya raia wa eneo hilo.
Katika kipindi cha miaka hiyo yote waasi hao waliua mamia ya watu katika eneo la Beni.
Mwaka jana jeshi la DRC lilianzisha oparesheni kubwa dhidi ya ADF na kundi hilo nalo limekuwa likitekeleza hujuma za kulipiza kisasi dhidi ya raia.
Umoja wa Mataifa unasema yanayojiri katika eneo hilo yanaweza kutambuliwa kuwa ni jinai za kivita.
Kushindwa jeshi la Congo na kikosi cha MONUSCO kukabiliana na wanamgambo wenye silaha wakiwemo waasi hao kumepelekea kuongezeka ukosefu wa amani nchini humo khususan mashariki mwa nchi.