Wasema atafuata nyayo za Dk. Shein

NA AMEIR KHALID

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilimchagua Dk. Hussein Ali Mwinyi kupeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya urais wa Zanzibar.

Mkutano huo ulifanyika Dodoma ambapo Dk. Mwinyi aliibuka mshindi baada ya kuwashinda wanachama wengine walioingia hatua ya tano bora.

Hivyo basi mara baada ya uteuzi huo na uchaguzi utakaofanyika mwezi mwezi Oktoba, tayari wanamichezo wengi hivi wameanza kuwa na moyo wa tamaa ya kupata mambo mazuri kutoka kwa rais huyo ajae.

Chama cha mpira wa Mikono (Handball) kimeelezea matumaini yake makubwa kwa rais ajae ambapo, Katibu Mkuu wa chama hicho Mussa Abdurabi Fadhil, alisema matarajio ya chama kwa rais ajaye ni kuendeleza pale ambapo mtangulizi wake amefikia.

Alisema wanaimani kuwa ataendeleza jitihada za mtangulizi wake katika suala zima la usimamizi na uimarishaji wa michezo nchini akianzia ngazi ya chini katika skuli za msingi na sekondari hatimaye vyuo vikuu.

Pia alisema wanataka somo la michezo liendelezwe katika ngazi ya sekondari na msingi, lengo ni kupata wachezaji wenye taaluma ya michezo ambapo mtangulizi wake ameridhia somo hilo ambalo hivi sasa linafundishwa katika ngazi ya sekondari ya ‘A level’.

Kuimarika kwa mchezo ni pamoja na kuwepo kwa miundombinu bora ya michezo, wataalamu wa kutosha, vifaa. Hivyo ahakikishe miundombinu ya viwanja vya mchezo huu vinaimarishwa na kunapatikana angalau kiwanja kimoja cha ‘indoor’ kwa ajili ya michezo ya kimataifa.

Suala la upatikanaji wa vifaa vya mchezo huu nalo liwe ni chachu ya kuimarisha mchezo, pamoja na kuhakikisha kuwa wataalamu wa kutosha wanapatikana.

Michezo iwe ni miongoni mwa sera na ianzie katika ngazi za chini kabisa kwenye skuli za msingi, na ihakikishwe kunakuwa na chombo maalumu kitakachosimamia michezo chenye wasimamizi wanamichezo.

Michezo ni gharama hivyo ahakikishe kunakuwa na mfuko maalumu wa michezo utakaochangiwa na wadau mbalimbali kupitia shughuli za kila siku za kiuchumi.

Michezo kwa ujumla amelisimamia ipasavyo ingawa alitoa kipaumbele kwa michezo lakini hilo ni jambo la kawaida, lazima katika kupata mafanikio uwe na vipaumbele. Lakini hakuna mchezo ambao ulikosa fursa katika utawala wake.

Kuliweka somo la michezo katika skuli za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, jambo ambalo awali halikuwepo na hivi sasa kwa mafanikio makubwa limeanza ngazi ya ‘A level’.

Uanzishaji wa viwanja vya michezo katika wilaya (Multipupose) ni jitihada za kuimarisha michezo nchini kwetu.

Hata hivyo alisema katika kipindi hiki chama chake litaka kuwaendeleza walimu na waamuzi waliopo, kuandaa ‘startegic plan’ yake na action plan, kuandaa mashindano ya kimataifa.

Kuurejesha mchezo katika skuli za msingi na sekondari. Pia walipanga kutafuta wadhamini na wahisani wa kukisaidia chama kuyafikia malengo yake.

Hata hivyo mbali na changamoto hizo katika kipindi cha miaka 10 mambo kadhaa walifanikiwa kuyaendesha, ikwa ni pamoja na kuandaa mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, kutoa mafunzo kwa walimu wa mchezo, kuandaa ‘startegic plan yake na ‘action plan’.

Kutafuta misaada mbalimbali kwa wadau nje ya Zanzibar ambapo wamefanikiwa kupata mtaalamu kutoka Ujerumani, hivyo amemuomba rais mtarajiwa kusaidia kuyafanikisha mambo hayo ambayo walishindwa kuyatimiza.

Wasanii nao hawakuwa mbali katika kutoa maoni yao juu ya matarajio ya rais ajaye ambapo walimshauri Dk. Hussein mara baada ya kupata ridhaa ya wananchi wa Zanzibar ni vyema kufuata nyayo za Rais atakaeondoka madarakani Dk. Ali Mohamed Shein kuwa karibu nao.

Walisema kwamba Dk. Shein amekuwa mstari wa mbele katika kusukuma gurudumu la wasanii na wanamichezo kutokana na wao kuwa kioo cha jamii katika mambo mbali mbali.

Wasanii hao waliomba Dk. Hussein mara baada ya kupata ridhaa ya Wazanzibari asiwasahau wasanii, afuate mguu wa Dk. Shein kwa sababu yeye alikua nao bega kwa bega katika kufanikisha kazi zetu zinafanyika.

Walisema ni vyema Dk. Hussein akipata nafasi ya kuiongoza Zanzibar kwa nia njema awafanyie mambo mengi mazuri ya wasanii.

Kwa upande wa wanamichezo wa soka walisema katika kipindi cha uongozi wa Dk. Shein sekta ya michezo iliimarika sana kwani aliweza kufufua michezo na kuendeleza mambo mbali mbali mazuri kupitia fani hiyo.

Walisema michezo ni moja ya jambo ambalo wananchi wanapenda hivyo ni vyema kwa kiongozi huyo mtarajiwa awe karibu katika kufufua michezo mbali mbali, pamoja na kukutana na wanamichezo kwa kupeana ushauri ambao utasaidia nchi kupata maendeleo kupitia sekta hiyo.

Kwa upande wa soka Ali Ame wa Shaurimoyo alisema wanamichezo waliridhishwa na mafanikio ya Dk. Shein katika michezo hasa wa soka, lakini tatizo la baadhi ya watendaji wa vyama ndio walioangusha soka la Zanzibar na kusababisha mizozo.

Alisema kuna viongozi ambao wana nia ya kweli ya kuendeleza soka lakini wanarejeshwa nyuma na watu ambao wapo kwa maslahi yao.

‘’Dk. Shein kajitahidi bado kuna changamoto nyingi kwenye mpira ikwemo kukosekana wadhamini, ukosefu wa wawasimamizi wazuri katika soka’’, walisema.

Hivyo wamemuomba Dk. Mwinyi kuhakikisha analifanyika kazi suala hili kwa kuwachukulia hatua viongozi ambao hawana lengo la kuongoza mpira wa miguu lakini wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

Hivyo basi wametoa ushauri kwa rais ajae kuwa makini na kufuatilia kwa makini mwenendo wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) ambao haupo vizuri.

 Abdalla Juma wa Meli Tano alisema rais ajae azidi kuendeleza aliyoyaacha ikiwemo kuwapa hamasa zaidi, kuendelezwa viwanja vya ndani ili vijana waweze kuonesha vipaji vyao.

Ali Khamis Machenga alisema Dk. Shein aliweka miundombinu mizuri ya soka ingawa haijakamilika, hivyo rais ajae wanamuomba aweke bajeti maalumu kusaidia klabu na kukuza vipaji vya vijana.

‘’Serikali itie mkono wake ili kupata wadhamini wa ligi yao kwani mpira bila pesa hauwezi kuwa mzuri’’, alisema.

Abdulmutrik Kiduu alisema wanamichezo hivi sasa wanataka viongozi bora wakaoweza kuendesha vyema bila ya mizengwe, hivyo ni rais ajae wanamuomba kuchagua viongozi wanaojua michezo.

Wanamichezo wa mpira wa Wavu walisema wanamategemeo makubwa zaidi kutoka kwa Dk. Hussen Mwinyi katika kuendeleza mchezo huo ambao hivi sasa unafanya vizuri.

Walisema wanaimani kuwa ndani ya miaka mitano ya mwanzo atajenga uwanja maalum wa michezo ya aina hiyo (Indoor game) Unguja na Pemba.