NA HABIBA ZARALI

WANANCHI wa wilaya ya Mkoani, wameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein, kwa

hatua kubwa iliochukua ya kuirejeshea hadhi hoteli ya serikali Mkoani jambo ambalo litakuza uchumi sambamba na pato la wananchi.

Hoteli hiyo ambayo ilifanyiwa matengenezo makubwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) imeanza kuiletea haiba kubwa wilaya hiyo kwa kuwa na sura mpya pia baadhi ya wananchi watakuza vipato vyao na kupambana na umaskini.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, walisema hoteli hiyo  itasaidia kupunguza tatizo la malazi kwa wageni wanaofika katika kisiwa hicho.

Walieleza kuwa juhudi zilizofanywa na ZSSF ni za kuigwa kwani kunatoa ushindani wa kibiashara na kupatikana maendeleo endelevu ndani ya wilaya hiyo.

Ali Mohammed,mkaazi wa Mkoani alisema ni muda mrefu  mji huo ulikosa hoteli kubwa  na yenye hadhi nzuri na kulazimika kuwasafirisha wageni hadi mji wa Chake Chake.

Alisema kutokana na kuwepo hospitali na bandari kuu ndani ya mji huo, hoteli hiyo itasaidia kuwahifadhi wale wenye mahitaji ya sehemu ya kupumzika.

Akizungumzia ajira alisema ana imani kubwa ya kuwa wijana wa Mkoani watafaidika  kwa kupata ajira zitakazowawezesha kuendesha maisha yao.

Nae Bakar Muhammed Abeid, alisema mbali na ajira, lakini  kuwepo kwa hoteli hiyo pia mji wa Mkoani utanawirika kwa mafanikio yatakayopatikana kupitia sekta ya hiyo.

Alishauri kila mmoja kuchukua tahadhari kwa kuitunza vizuri ili iweze kuleta faida endelevu na kuepusha kuleta tena tabu kama iliokuwepo mwanzo.

Hija Hassan Hija,mkaazi wa Chokocho alisema kuwepo kwa hoteli hiyo katika mji wa Mkoani ni kitu cha faraja na cha kujivunia kwani itaondosha changamoto mbali mbali zilizokuwepo.

Alieleza kuwa hiyo ni fursa kwa vijana wenye uzoefu wa masuala ya hoteli kuweza kutumia vipaji vyao kwa kufuatilia  kuomba ajira kwani hiyo ndio mkombozi kwao.

Amour Omar Ngwali  mkaazi wa Mkoani, aliiomba ZSSF kuwaletea maendeleo zaidi wananchi ikiwemo uwekezaji wa majengo mbali mbali yenye hadhi.

“Kuwepo kwa majengo yenye hadhi kama hili ndani ya wilaya yetu ya Mkoani kutaiwezesha kuwa na mabadiliko ya mandhari ya mji kama ilivyo leo mji wa Gombani Pemba,” alisema.

Ufunguzi wa hoteli hiyo ni miongoni mwa ziara alioifanya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein

 kisiwani Pemba, ambapo wilaya ya Mkoani ilikosa hoteli kama hiyo kwa muda mrefu tokea kuondoka kwa Hoteli za Serikali zilizokuwepo katika miji mitatu ya Pemba.