NA HANIFA SALIM, PEMBA 

WANANCHI wa Kangani Wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba, wamesema kuanzishwa kwa kamati ya ulinzi shirikishi (Polisi jamii), ndani ya kijiji hicho, imeondoa kwa asilimia 80 matendo maovu ikiwemo wizi, uhalifu na uuzaji wa dawa za kulevya.

Seif Mohamed Said mkaazi wa Kangani alisema, katika kijiji hicho walikua na kilio kikubwa katika masuala ya wizi, ikiwemo kuku, Ng’ombe, ndizi, ingawa baada ya kuanzishwa kwa kamati hiyo, imepelekea kuzalisha mazao ikilinganishwa na zamani.

“Tumefanikiwa kupitia hili na tunashukuru sana kwani tulikua sehemu za mabondeni hatusubutu kwenda kutokana na makundi maovu yaliyoanzishwa na vijana, lakini kamanda wetu umetusaidia kazi kubwa ambayo imetufanya kuwa na amani katika maisha yetu,” alisema.

Akizungumzia suala la sheria alisema, kesi za ubakaji, uuaji na dawa za kulevya ni kesi ambazo hazina dhamana hadi pale zinapofika mahakamani, lakini kuna baadhi ya vijana walikamatwa wamerudi mitaani na kesi zao bado hazijafika mahakamani.

Katibu wa kamati ya kusimamia maadili polisi jamii Kangani Bakar Masoud Hamad alisema, dhima kubwa ya kuundwa kamati hizo, ni kusimamia maadili kwa watu wote, ikiwemo vijana na watoto, ingawa bado wazazi hawajaona umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

“Tunakuomba kwa Jeshi la Polisi katika suala hili tushirikiane, kulisimamia na kuhakikisha watoto tunawarejesha skuli, hili lisifanyike kwa hiari bali kwa nguvu zote za kipolisi kwani wanapokaa bila ya kusoma ndipo wanapoanza masuala ya wizi,” alisema.

Aidha, aliliomba Jeshi la polisi ikiwa kutakua na kanuni ndogo ndogo za kuweza kuwadhibiti watoto ambao wataki kusoma wawapatie mtaala, ili kujua namna gani wanautumia kwani alisema, watoto hao ndio wanaoanza kuvuta unga baada ya kubaki mitaani.

Nae Kasim Haji Salim alisema, kwa upande wake anaunga mkono kwa asilimia 100 juhudi zilizochukuliwa na Jeshi la polisi, kuweza kukabiliana na uhalifu ndani ya shehia yao.