NA FATMA AYOUB, MCC

WANANCHI wametakiwa kufuata ushauri wa madaktari na wataalamu wa afya, ili kupunguza maradhi yanaweza kuepukika ndani ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Msaidizi Mkuu wa Kitengo cha elimu ya Afya, Abrahmani Kwaza, wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Sogea Mjini Magharibi Unguja.

Alisema kutokana na tathmini iliyofanywa imegundulika kuwa watu wengi wanasumbuliwa na maradhi ambayo yanaweza kuepukika yakiwemo yasio ambikiza kwa kufuata na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya.

Alifahamisha kuwa kuna maradhi ya aina mbili ikiwemo ya  kuambukiza na yasio ambukiza hivyo watu wengi wamekuwa wakisumbuliwa na maradhi ambayo hayaambukizi kwa kutozingatia kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.

 Hivyo, aliwataka wananchi kupunguza kutumia mafuta katika vyakula vyao na kupunguza kula vitu vya uanga na kufanya mazoezi mara kwa mara, kwani kutasaidia kuyeyusha mafuta mwilini.

“Watu wengi wamekuwa wakila vyakula vya mafuta na uwanga halafu hawafanyi mazoezi jambo ambalo linapelekea kuoengeza maradhi ikiwemo maradhi ya gesi” alisema.

Sambamba na hayo aliwataka  watu kutumia matunda kwa wingi, kunywa maji kwa na kupenda kutumia mboga mboga kwani kutasaidia sana kujenga afya na kujikinga na maradhi ya aina hiyo.

“Ili tuwe na afya bora tunatakiwa kutumia matunda kwani ndani yake kunakuwa na mchanganyiko wa vitu mbalimbali” alisema.