NA HAJI NASSOR

WANAFUNZI wamekumbushwa kuwa mkopo kwa ajili ya elimu ya juu unaotolewa na bodi ya mikopo, hapewi kila mtu bali unatolewa kwa kuzingatia vipaumbele vya nchi ili watakaohitimu wakubalike katika soko la ajira.

Hayo yalielezwa na Kamishna wa idara ya watendakazi kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, Salama Ramadhan Makame, alipokuwa akizungumza na wahitimu na wanafunzi wa kidato cha sita katika skuli ya sekondari Chasasa wilaya ya Wete.

Alisema, serikali baada ya kufanya utafiti iligundua kuwa ilikuwa ikisomesha wataalamu wa fani moja pekee lakini baadaa ya kugundua hilo, sasa imeamua kuangalia soko la ajira lilivyo.

Alisema hapo awali, kulikuwa na makundi ya wahitimu hasa wanasheria na wahasibu huku wataalamu wengine wakiwemo wa mafuta na gesi wakikosekana.

Alisema kila mmoja ana haki ya kuomba mkopo lakini sio kila muombaji anaweza kupewa kutokana na serikali kuweka vipaumbele vyake.

“Sasa huwezi kupewa mkopo kama kwenye vipaumbe vye serikali huna sifa, kwani sasa tunatoa na kusomesha wanafunzi wa fani ambazo Zanzibar bado ni adimu ikiwemo waalimu wa sayansi na madaktari,”alieleza.

Alivitaja, baadhi vya vipaumebele hivyo kuwa ni pamoja na wataalamu wa chambuzi wa ardhi, wataalamu wa upandikizaji mbegu, miti, utibabu wa wanyama na mimea.

Eneo jengine ambalo aliwataka waombaji kulichangamkia kuwa ni sekta ya utalii, mafuta na gesi, wataalamu wa dawa za usingizi, meno, ubongo, viungo, sikio, pua, macho na koo pamoja na wahandishi wa maji.

Mapema Ofisa Habari wa bodi hiyo, Khamis Haji Omar, alisema miongoni mwa nyaraka zinazotakiwa kwa muombaji, ni kitambulisho cha mzanzibari mkaazi.

Alisema pia awe na cheti cha kumalizia masomo ya kidato cha nne au sita, wadhamini wawili na kuzingatia vipaumbele vya nchi ambavyo vimeteuliwa.

“Mkopo wa elimu ya juu unaotolewa na bodi yetu, hauna riba hata kidogo, unaweza kuutofautisha na mikopo mengine ya kibiashara, hivyo haya ndio matunda ya serikali yetu,”alieleza.

Aliwaomba wanafunzi kuchangamkia haraka muda ambao umetolewa na bodi hiyo wa kuomba mikopo ili waendelee kutafuta ya elimu ya juu.

Nae Ofisa TEHEMA wa bodi hiyo, Abdalla Haji Faki, alisema kuanzia mwaka huu wa masomo, waombaji watatakiwa kuomba mikopo kwa njia ya kielektroniki kupitia zalos.zhelb.go.tz/zolas.

Aliwataka wanafunzi kuacha utamaduni wa kuomba mikopo kwenye bodi mbili kwani inaweza kusababisha usumbufu.

Nao wanafunzi wa skuli ya Chasasa, walisema ni vyema mtandao huo wa bodi ukawekwa sawa kila wakati ili waombaji wasikumbane na changamoto.