Wasema teuzi zake zitazingatia jinsia

NA HUSNA MOHAMMED

ZANZIBAR na Tanzania kwa ujumla zikielekea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu, wanawake wana matumaini makubwa ya kupata nafasi mbalimbali za uteuzi.

Katika hatua ya awali hasa wa chama tawala cha Mapinduzi, imeonesha kuwa licha ya wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za wabunge, uwakilishi na udiwani hata hivyo ni wachache mno waliopenya hatua ya mchujo.

Hivyo, makala haya inazungumza na vyanzo mbalimbali vya kundi la wanawake ili kuona wana matumaini gani kwa rais mteule kupitia Chama cha Mapinduzi iwapo atashinda kwenye uchaguzi mkuu atakavyotumia nafasi zake za uteuzi kuwainua wanawake.

MITAZAMO YA WANAWAKE WANA SIASA

Akizungumza na gazeti hili kuhusiana na maoni juu ya mgombea wa CCM, Dk. Hussein Mwinyi kwa wanawake katika nafasi za uongozi na huduma za kijamii kwa ujumla.

Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake Tanzania Zanzibar (UWT), Tunu Juma Kondo, alisema kwa mara ya kwanza wanawake wamehamasika kujitokeza kwa wingi katika nafasi hizo lakini inakatisha tamaa hasa nafasi za majimbo zilizopatikana kwa wanawake.

“Wanawake wengi walihamasika kuingia majimboni lakini wengi wametupwa kwenye hatua za awali za kura za maoni, lakini tuna matumaini rais atatuona pamoja na makundi mengine yaliyopembezoni ambayo yameachwa nyuma siku nyingi”, alisema.

“Kwa mfano tulitaka wagombea viti maalum wakae vipindi viwili lakini haikukubalika kutokana na utendaji wa wateuliwa kuwa mzuri na wanachama kuwakubali, kwa sababu unaweza kuchagua mtu mwengine na baadae akawa si mtendaji”, alisema.

“Tumeona mwanga mzuri kwa Rais anaemaliza muda wake, Dk. Ali Mohamed Shein namna alivyowasogeza wanawake na hili halina budi litafanyika kwa rais ajae”, alisema.

Kuhusiana na huduma za kijamii ambao wanawake ndio walengwa wakubwa alisema ataimarisha zaidi mbali na alipofika mtangulizi wake ambae ameimarisha mambo mengi ya kijamii.

Alisema wanawake wanapaswa kunufaika na huduma ya maji safi na salama, nishati ya umeme, huduma za afya za watoto na akinamama, miundombinu ya barabara na mengineyo mambo ambayo yametekelezwa kwa vitendo na awamu inayomalizika.

Tunu alieleza kuwa rais ajae hatakuwa na kazi sana kwa maeneo hayo, ila atalazimika kuimarisha zaidi ustawi wa wanawake na watoto.

Kwa upande wake Salma Saadat, ambae ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) aliipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Chama cha CCM kwa kumsimamisha mgombea Hussein Ali Hassan Mwinyi, ambapo anaamini kuwa atafanya vyema kwenye kazi yake hiyo.

“Tunaamini ustawi wa wanawake atauzingatia kwa staili yake keki ya taifa kwa viongozi wote tutaila pamoja na kama yeye amefuata nyayo za Rais Magufuli naamini hilo pia atalifanya”, alisema.

Aidha alisema kwa kuwa hali ya wagombea wanawake majimboni na nafasi zaawali za mchujo haiku vizuri anaamini kuwa rais ajae atatumia vyema nafasi yake kuwavuta wanawake kwenye nafasi za uongozi.

Kwa upande wake Salma Saadat, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu (JUWAUZA), alisema kuwa watu wenye ulemavu wana matumaini na Rais mteule wa chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi akichaguliwa kuwa rais wa Zanzibar.

“Wanawake, watu wenye ulemavu ni miongoni mwa makundi yaliyoachwa nyuma miaka mingi, ni wazi kuwa rais atawaona hasa akizingatiwa kuwa ni wa watu wote, wanawake wengi wameangushwa majimboni kwa nafasi zake atawapa nafasi za uteuzi”, alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa keki ya taifa italiwa na watu wa makundi yote kwa maana watafaidika sana na maendeleo ambayo anaamini hayatabagua jinsi ya mtu au kundi la mtu au hata mahala pa mtu.

“Tunaipongeza Serikali na chama tawala kumchagua mgombea huyu na wazanzibari wawe na imani kubwa ya kufikia malengo kuliko yaliyopo sasa tunaamini ni mtu mwema atakaeona shida za wananchi”, alisema. 

WASOMI

Nae Mgeni Hassan Juma, ambae pia ni Naibu Spika wa Baraza la wawakilishi Zanzibar, yeye alisema hana wasiwasi na Dk Hussein Mwinyi, kama atakuwa rais wa Zanzibar.

“Kwa kweli nnavyomfahamu Dk. Mwinyi wanawake sasa watazidi kupata mwelekeo mkubwa hasa katika kupunguza umaskini kwa kuwa anapenda sana kusaidia vikundi vya akinamama na SACCOS kwa ujumla wake”, alisema Mgeni.

Dk. Mwinyi ni mzalendo, mwadilifu, mpenda watu wanawake tutegemee neema kutoka kwake na atawaangalia kama chachu ya kuleta maendeleo ya nchi”, alisema.

Aidha alisema kuwa ataangalia sera, sheria na mitazamo ambayo inawakandamiza wananchi na kuifanya kuwa rafiki kwao ili nao waweze kusonga mbele.

Kuhusu nafasi za uongozi alisema kwa kuwa wanawake wengi wamejitokeza katika ngazi mbalimbali za uongozi kwenye kuomba ridhaa za kuchaguliwa lakini kwa bahati mbaya wameshindwa ni wazi hilo atalifanyia kazi.

WANANCHI WA KAWAIDA WANAMZUNGUMZIAJE

Asha Hamad (71) mkaazi wa Amani yeye alisema kuwa anaamini kuwa rais mpya ajae ataweza kuleta mabadiliko makubwa kwa wanawake kama ilivyo kwa Dk Shein au zaidi yake.

“Uongozi wa Dk. Shein umewaona sana wanawake kiasi kwamba leo hii tunajivunia mambo mengi yaliyokuzwa kupitia utawala wake”, alisema.

Alitolea mfano kwa viongozi wengi serikalini wanawake wamechaguliwa kwenye uongozi wake.

Nae Hamida Haji Kassim (34), mkaazi wa Shaurimoyo alisema ana matumaini kuwa rais mpya ajae atafanya mambo makubwa yanayowahusu wanawake.

“Kwa kweli sisi wanawake tunachangamoto kubwa za kisiasa, kiuchumi na kijamii tunaamini huyu Dk Hussein ataleta mabadiliko zaidi hasa kwa kuwachagua viongozi wanawake kwa nafasi mbalimbali za taasisi za umma, hili litatufanya wanawake kufikia lengo la 50 kwa 50”, alisema.

Nae Hidaya Ali Khamis (25) mkaazi wa Fuoni alisema kuwa kama yeye kijana anaamini kuwa Rais ajae Dk. Hussein Mwinyi nae ni kijana ataliona kundi hili kwa umuhimu wake.

“Vijana ndio wanaotegemewa kwa taifa la sasa na la baadae kiongozi huyu kijana anayajua sana matatizo ya vijana tukae tayari kumpa ushirikiano hakuna lisilowezekana”, alisema.

Aliswataka wazanzibari kubadilika na kuwa na maono ya mbali na kusema kuwa maendeleo zaidi yanakuja hivyo ushirikiano unahitajika kufikia huko.

Ni wazi kuwa kupitia maoni ya watu mbalimbali juu ya kumpokea Rais mratajiwa Dk. Hussein Mwinyi wanategemea maendeleo makubwa iwapo wananchi watampa ridhaa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.