RAMALLAH, PALESTINA
HARAKATI za mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imewataka Wapalestina wote kutetea na kuulinda Msikiti mtakatifu wa al Aqsa na kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya msikiti huo.
Msemaji wa Hamas, Abdul-Latif al-Qanu alisema kuwa, hatua za kiuadui za utawala wa Israel dhidi ya mji mtakatifu wa Quds na mashambulizi ya jeshi la utawala huo katika Msikiti wa Aqsa sambamba na ujenzi wa maelfu ya nyumba za Waisrael katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina ni hatari kubwa kwa Wapalestina na msikiti huo.
Al-Qanu alisema kuwa, hatua hizo za Israel zina lengo la kuwafukuza Wapalestina katika makaazi yao na hatimaye kuudhibiti kikamilifu Msikiti wa al Aqsa.
Siku chache zilizopita utawala wa Israel ulizindua mpango wa kujenga maelfu ya nyumba za Waisrael katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds.
Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kibaguzi na uliozinduliwa na Rais Donald Trump wa Marekani tokea tarehe 28 Januari mwaka huu.