GITEGA,BURUNDI

WATU 15 wameuawa baada ya watu waliojidhatiti kwa silaha kushambulia wakaazi wa eneo moja huko kusini mwa Burundi.

Haijabainika iwapo waliouawa katika shambulizi hilo kama ni wakaazi wa eneo lililoshambuliwa,waasi walioshambulia au maofisa usalama.

Taarifa zinaeleza kuwa,Wilaya ya Bugarama iliyoko katika mkoa wa Rumonge kusini mwa Burundi inashuhudia mapigano makali, na vita hivyo viliendelea hadi Jumatatu.

Mmoja wa mashuhuda wa shambulizi hilo alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa,watu waliobeba bunduki waliwateka wakaazi waliokutana nao na kisha kuwaua kabla ya kutokea makabiliano makali baina yao na askari jeshi.

Ofisa mmoja wa Serikali ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema mashambulizi ya namna hiyo yalitarajiwa kuanzishwa na waasi wanaopinga mpango wa Serikali wa kuanza kuwarejesha nchini wakimbizi raia wa nchi hiyo walioko Rwanda.

Rwanda ni mwenyeji wa maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi,waliokimbia vita na mapigano nchini kwao tokea mwaka 2015.