BAKAR MUSSA, PEMBA

WASIMAMIZI wa Uchaguzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ngazi ya majimbo  Kisiwani Pemba, wamesisitizwa  kuendelea kusoma sheria za uchaguzi , kanuni na maelekezo mbali mbali yaliotolewa na Tume hiyo ili yawaongoze katika kusimamia  uchaguzi wa haki na huru.

Akifunga mafunzo kwa Watendaji hao Makamo Mwenyekiti wa Tume hiyo , Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Mbarouk Salim Mbarouk, huko katika ukumbi wa Kiwanda cha mafuta ya Makonyo Wawi Chake Chake Pemba, alisema njia pekee ya kufanikisha zoezi hilo ni kwa watendaji hao kufuata misingi ya sheria na Kanuni za Uchaguzi  kuliko kutumia uzoefu walionao.

Alieleza pamoja na kwamba uzoefu ni nyenzo muhimu katika kufanikisha Uchaguzi , lakini pia unaweza kuwaponza kwa kufikiria kuwa wanajuwa kila kitu na kusahau kujisomea kile walichofundishwa.

Aliwataka kufahamu kwamba jukumu kubwa liliopo mbele yao ni kuwateuwa na na kuwapatia mafunzo kwa watendaji  wa vituo watakao wateuwa  katika Wilaya zao kwa kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa mustkabali wa Taifa la Tanzania.

Aidha Jaji Mbarouk , aliwahimiza Wasimamizi hao wa Uchaguzi kutumia vyema mbinu , ujuzi na elimu walioipata  ili ujumbe uliomo katika mafunzo mutakayo wapatia yanawafikia Walengwa.