NA ASYA HASSAN

WAZAZI wameshauriwa kuongeza nguvu katika kupambana na kuvidhibiti vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto vinavyojitokeza nchini.


Wito huo ulitolewa na wanaharakati wa kupambana na vitendo hivyo walipozungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni walipokuwa wakishiriki mafunzo kuhusu masuala ya kijinsia.

Mafunzo hayo ni utekelezaji mradi wa miaka miwili juu ya kuwawezesha waathirika wa vitendo vya udhalilishaji ili waweze kufatilia kesi zao hadi mwisho unaotekelezwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) ofisi ya Zanzibar.


Walisema wazazi wana nafasi kubwa juu ya kudhibiti vitendo wanavyofanyiwa watoto wao, hivyo ni vyema kuwa tayari na kuongeza nguvu kushirikiana na serikali ili kuviondoa.


Mwanaharakati Hija Masoud Ame, kutoka mkoa wa Kusini Unguja, alisema wazazi wanapaswa kujua kuwa wana wajibu wa kushirikiana na serikali katika mapambano, kupinga na kuvikomesha vitendo hivyo ambavyo vimekua vikiendelea kuiathiri jamii na kulitia doa taifa kutokana na matendo hayo kuendelea kufanyika nchini.


Alisema hadi sasa wana kesi 15 wanazozifatilia ambazo baadhi yao zipo
mahakamani na nyengine katika vituo vya polisi zikiendelea na upelelezi.

Kwa upande wake Hadia Ali Makame kutoka mkoa wa Kaskazini Unguja,  alisema elimu inayotolewa imesaidia jamii kuwa na mwamko wa kuripoti kesi hizo pale zinapotokea lakini hawazifatilii mpaka mwisho hali ambayo inatoa nafasi kwa wafanyaji kuendeleza matendo hayo.

Aidha alitumia fursa hiyo kuitaka jamii kuwa wawazi na kuondokana na
muhali na badala yake kuviripoti vitendo hivyo katika sehemu husika
ili wafanyaji waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Sambamba na hayo alifahamisha kwamba bila ya kuwepo mashirikiano ya pamoja baina ya jamiii na serikali vitendo hivyo haviwezi kuondoka na jamii itakuwa inaendelea kuathirika.


naye ofisa ufatiliaji wa miradi na tathmini wa TAMWA Mohammed Khatib Mohammed, alisema katika kupambana na vitendo hivyo chama chake kimekuwa kikisimamia miradi kadhaa na kufanya harakati mbalimbali ikiwemo ya kutoa elimu kwa jamii ili kuwa na ujasiri wa kuripoti na kuzifatilia kesi hadi hatua ya mwisho ili wafanyaji watiwe hatiani.