NA ASYA HASSAN

MAHAKAMA kuu Vuga, imewaamuru washitakiwa wawili waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya fedha za ofisi, kurudisha serikalini ndani ya miezi mitatu mamilioni ya fedha baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya.

Akisoma hukumu kwa washitakiwa hao, Jaji wa Mahakama kuu Abraham Mwampashe, alimtaka mshitakiwa Said Ali Makame (48) mkaazi wa Amani kwa wazee Unguja, kurudisha fedha shilingi 38,415,000.

Mshitakiwa mwengine alipewa adhabu hiyo ni Othman Hussein Othman (60) mkaazi wa Bububu, ambaye yeye alitakiwa kurudisha shilingi 35,415,000 walizogawana ikiwa ni mali ya serikali.

Mbali ya hatua hiyo, pia mahakama hiyo imewataka washitakiwa hao kulipa faini ya shilingi 2,500,000 pamoja na kutaifishwa gari mbili aina ya Noah na Super Custom zinazomilikiwa na watu hao.

Jaji Abraham Mwampashe, alitoa adhabu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliyowasilishwa na upande wa mashitaka.

Hata hivyo mahakama ilisema kuwa, ikiwa washitakiwa hao watashindwa kulipa fedha hizo basi mahakama itatoa maamuzi mengine dhidi yao. 

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na kosa la matumizi mabaya ya ofisi, kinyume na kifungu cha 53 cha sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar namba 1 ya mwaka 2012.

Ilidaiwa mahakamani hapo, Said Ali Makame ambae ni mkuu wa kitengo cha deni la taifa wizara ya fedha na Mipango, mnamo mwezi Oktoba hadi Novemba akiwa katika majukumu yake ya kazi, alijipatia faida isiyo halali ya kiasi cha shilingi 87,243.667.

Fedha hizo alidaiwa kujipatia kwa makusudi kwa ajili ya kuidhinisha malipo ya kiinuua mgongo cha marehemu Chumu Hassan Chum, ambazo zilikua zimeshalipwa kwa warithi wake tangu mwaka 2017 kupitia kesi ya mirathi nambari 39/2017.

Hati hiyo ilidai kuwa, mshitakiwa Othman Hussein Othman, kwa makusudi aliwasaidia Juma Abdalla Othman na Said Ali Makame kutengeneza na kuandaa warithi na wadai wasio halali, kwa kufanya malipo ya shilingi 87,243.667 ya kiinuua mgongo ya marehemu Chumu Hassan Chum, ambazo zilikua zishalipwa kwa warithi wake tangu mwaka 2017 kupitia kesi ya mirathi nambari 39/2017.

Juma Abdalla Othman Mkaazi wa Chumbuni (52) ambae ni karani wa Wakfu na Mali Amana Zanzibar, mnamo mwezi Oktoba hadi Novemba akiwa katika majukumu yake ya kazi aliitumia nafasi yake vibaya.

Alidaiwa kuwa, Juma alidaiwa kuandaa fomu ya mirathi (TIRKA) kwa madhumuni ya kujipatia faida isiyo halali  kiasi  cha shilingi 87,243.667 malipo ya kiinuua mgongo  ya marehemu Chumu Hassan Chum, ambazo zilikua tayari  zishalipwa kwa warithi wake tangu mwaka 2017 kupitia kesi  ya mirathi nambari 39/2017.

Ilidaiwa kwamba mahakamani hapo, hukumu dhidi ya mshitakiwa Juma Abdalla Othman, itasikilizwa Septemba 14 ya mwaka huu kutokana na siku hiyo hakuhudhuria mahakamani hapo kwa sababu alikuwa anaumwa.

Kabla ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Shamsi Yassin Saad, alidai upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuiomba mahakama hiyo itowe adhabu kwa mujibu wa sheria, ili iwefundisho kwao na watu wengine wenye tabia kama hiyo juu ya matumizi mabaya ya ofisi.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa ajili ya kusomewa mashitaka yao.