NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema vyama vya siasa 16 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu, vimetoa wanachama waliochukua fomu kwenye tume hiyo kuomba uteuzi wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha Tume na wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Mahela Charles alisema kuwa kesho chama cha NLD kinatarajia kuchukua fomu ambapo kitabaki chama cha UDP na TLP.

Dk. Charles alisema vyama ambavyo havijachukua fomu ni UDP na TLP ambapo Agosti 25 mwaka huu ndio mwisho wa zoezi la uchukuaji wa fomu ya kugombea Urais.

Awali akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema kuelekea uchaguzi mkuu Tume imeandaa bajeti ya shilingi bilioni 331,728,258,035.00.

Jaji Kaijage alisema kwa kuzingatia kifungu cha 122 cha sheria ya taifa ya uchaguzi, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mfuko mkuu wa hazina ambapo itagharamia shughuli zote za uchaguzi kwa asilimia 100.

Aliongeza katika eneo la vifaa vya uchaguzi Tume inaendelea na mchakato wa ununuzi wa vifaa sambamba na uchapishaji wa fomu, sheria za uchaguzi, kanuni na maelekezo.

Alibainisha katika awamu zote mbili, uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ulifanyika katika vituo 37,814 vya kuandikisha wapiga kura wapya 7,326,552 sawa na asilimia 31.63 ya wapiga kura 23,161,440 walioandikishwa mwaka 2015.

Alifafanua kuwa jumla ya wapiga kura 3,548,346 waliboresha taarifa zao na wapiga kura 30,487 waliondolewa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kutokana na kukosa sifa.

Alisema baada ya kuwaondoa wapiga kura ambao taarifa zao zimejirudia kwa hivi sasa daftari lina jumla ya wapiga kura 29,188,347, hivyo kutokana na idadi hiyo katika uchaguzi mwaka huu kutakuwa na vituo 80,155 vya kipiga kura.

Aidha alisema katika maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka huu, hakutakuwa na marekebisho katika sheria za uchaguzi, ambapo tume imefanya maboresho ya kanuni za uchaguzi wa Rais, na Wabunge, za mwaka 2020 na kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa, (uchaguzi wa madiwani) za mwaka huu.