KINSHASA,CONGO

WATU  wasiopungua 13 wameuawa katika shambulio lililofanywa na waasi wa kundi la The Allied Democratic Forces (ADF) kutoka Uganda huko mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mashambulizi hayo ni katika mlolongo wa mauaji yanayoendelea kufanywa na kundi hilo ambayo Umoja wa Mataifa unasema kuwa inaaminika kuwa ni jinai ya kivita.

Mkuu wa kijiji cha Kinziki Matiba na Wikeno,Chui Mukalangirwa, alisema kuwa waasi hao waliwafunga kamba wanavijiji kabla ya kuwaua Ijumaa ya jana.

Chui Mukalangirwa aliitaka Serikali kukomesha uhalifu na umwagaji damu katika maeneo hayo.

Msemaji wa Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo alithibitisha mauaji hayo na kusema, jeshi hilo limewasaidia raia kuzika wahanga wa shambulio hilo.

Antony Mwalishayi alisema, jeshi limepeleka idadi kubwa ya askari katika eneo hilo kwa ajili ya kulinda usalama. 

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, kundi la waasi wa ADF kutoka Uganda limeua zaidi ya raia elfu moja katika mkoa wa Kivu Kaskazini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu mwaka jana wa 2019. 

Mashambulizi yanayoendelea kufanywa na kundi hilo huko mashariki mwa Congo DR yaliwalazimisha maelfu ya watu kukimbia makaazi yao na kutatiza juhudi za Serikali za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona na ugonjwa wa Ebola ambao umeua zaidi ya watu 2,200 nchini humo.