KINSHASA, DRC

WATU wasiopungua 40,000 wamekimbia machafuko ya kikabila katika eneo la milimani la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo limesema linatoa msaada muhimu wa kibinadamu.

Katika taarifa yake UNICEF ilisema,watu hao zaidi ya 40,000 wanajumuisha watoto 7,500 wa umri wa chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito zaidi ya 1,500, na walikimbia kutoka katika vijiji vilivyoko Uvira, Fizi na Mwenga wengine tangu mwezi Mei kutokana na mapigano ya kikabila ambayo yaliathiri maisha ya maelfu ya watu.

Katika machafuko hayo UNICEF inakadiria kwamba vituo kumi vya afya viliporwa na kuharibiwa kiasi cha kutoweza kutumika huku vituo vyengine 18 vikitelekezwa na wahudumu wa afya waliokimbia kulinda usalama wao.

Takriban skuli 28 ziliharibiwa mwezi Desemba mwaka 2019 na hadi sasa hazijajengwa upya hivyo huwaacha maelfu ya watoto bila mahala pa kusomea katika jimbo hilo.

UNICEF na wadau wake kwa sasa wanajikita kwa kazi na msaada wao katika eneo la Mikenge ambako watu 40,000 walipata hifadhi katika maeneo ya porini ambako si mbali  na maeneo walikotoka.

UNICEF ilionya kwamba hali ni mbaya sana kwa watu waliotawanywa katika milima ya Kivu Kusini wakihitaji haraka chakula, malazi, huduma za afya na msaada wa elimu, hivyo shirika hilo limetoa wito kwa wadau wa misaada ya kibinadamu kujitolea kusaidia haraka eneo hilo.

Ombi la fedha la UNICEF kwa ajili ya watoto wa DRC ni dola milioni 301 lakini hadi kufikia 15 Julai mwaka huu ni dola milioni 27,000 tu zilizopatikana na nyengine milioni 40 ni za mwaka jana hivyo kuacha pengo kubwa la dola milioni 219 sawa na asilimia 73 ya ombi lote.