JUBA,SUDAN KUSINI
UMOJA wa Mataifa umesema watu wasiopungua 70 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika makabiliano ya mwishoni mwa wiki kati ya wanajeshi na raia waliokataa kusalimisha silaha zao, kama sehemu ya makubaliano ya amani nchini Sudan Kusini.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric,alisema kwa kunukuu ujumbe wa umoja huo nchini Sudan Kusini, kuwa vurugu hizo zilisababishwa na tofauti kuhusu zoezi la kusalimisha silaha linalofanyika katika eneo la Romic.
Katika mazungumzo na shirika la habari la Ujerumani DPA, Diwani wa mji huo James Mabior Makuei, alisema makabiliano yalizuka baada ya wanajeshi waliokuwa kwenye doria kwenye eneo hilo, walipojaribu kuwanyang’anya silaha raia katika mji wa Tonj Mashariki, jimbo la Warrap, kama sehemu ya makubaliano ya amani yaliofikiwa hivi karibuni.
Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi Lul Ruai Koang, mapigano hayo yalisambaa haraka katika vijiji vya karibu, ambapo raia waliojihami waliivamia kambi ya jeshi katika mji wa Romic.