NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA
WATU wawili wamepoteza Maisha na wengine 19 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea eneo la njia panda ya Monduli ,Barabara Kuu ya Arusha Babati baada ya basi la kampuni ya Freys kugongana la Gari la abiria aina ya Coaster.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ,Salumu Hamduni, kwa waandishi wa Habari , ajali hiyo imetokea Jana Majira ya saa 8.40 mchana wakati basi la Frey’s lenye Namba T448 DDL aina ya Youtong likitokea Arusha kuelekea Singida.
Alisema basi hilo liligongana na Gari lenye Namba T 883 DEF aina ya Coaster lililokuwa linatokea Wilayani Monduli kwenda jijini Arusha baada ya Gari hilo kuingia ghafla barabara Kuu na kukutana na basi hilo.
Kamanda Hamduni, alisema kuwa waliofariki dunia hawakuweza kutambulika majina yao Mara moja, ila wanakadiliwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35 na mwingine mwenye umri wa miaka 25 hadi 35 wote walikuwa ni abiria wa Gari la Coaster .
Akizungumzia chanzo cha Tukio hilo Kamanda alisema ni kutokana na uzembe wa Dereva wa Gari la Coaster, ambaye hakufahamika jina lake Mara moja kuingia ghafla barabara Kuu akitokea Barabara ndogo ya Monduli na hivyo kukutana na basi la Frey’s lilitokea Arusha na kugongana.