NA RAJAB MKASABA, IKULU

KATIBU Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, amewataka viongozi na watumishi wa sekta ya umma kuacha kupiga siasa ofisini badala yake wachape kazi kwa bidii hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti, ikulu Zanzibar wakati viongozi wa wizara za serikali walipowasilisha taarifa za utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2019/2020 na ule wa mwaka 2020/2021 chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Aliwataka viongozi kuwasimamia watendaji wao ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Alisema ni kawaida kwa baadhi ya viongozi na wafanyakazi kujikita katika siasa katika kipindi kama hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na kusahau majukumu waliyopewa.

Aidha, alieleza kuwa viongozi na wafanyakazi wana wajibu wa kushirikiana na kusaidiana katika kipindi hiki kwani kuna mambo mengi yanatakiwa kutekelezwa.

Aliwatanabaisha viongozi kuwasimamia watendaji wao na kuwataka watambue kwamba uchaguzi isiwe sababu ya kuacha kutekeleza majukumu yao ya kazi.

Alisisitiza kuwa ni vyema watumishi na viongozi wa sekta ya umma wakaepuka mambo yanayokengeuka maadili ya kiutumishi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

“Waliotangaza nia tuwaache waendelee na sisi watumishi wa umma tuendelee kuchapa kazi,” alisisitiza.

Alisisitiza haja ya kuendelezwa utaratibu wa utayarishaji wa ‘bango kitita’ kwani una msaada kwa viongozi na watendaji katika kujitathmini kwenye utendaji wa kazi zao.

Aliwasisitiza viongozi hao kuendelea kushirikiana, kupendana  na kusaidiana miongoni mwao pamoja na kushirikiana na wale wanaowaongoza ili Zanzibar iendelee kupata mafanikio.

Aliwataka viongozi kutulia na kufanya kazi zao ipasavyo kwani kiongozi hupimwa kwa utendaji wake.