NA MASANJA MABULA , PEMBA

WAKAZI wa kijiji cha Minazini Shehia ya Tibirinzi wilaya ya Chake Chake wameanzisha msako wa nyumba hadi nyumba kuwasaka wauzaji  na watumiaji wa pombe haramu aina ya gongo pamoja na madawa ya kulevya.

Msako huo uliosimamiwa na polisi Jamii wa kijiji hicho ulifanikiwa kuwakamata vijana wawili wanaodaiwa kuwa ni watumiaji wa pombe haramu aina ya gongo na dawa za kulevya.

Mmoja wa kijana aliyekamatwa akituhumiwa kuwa mtumiaji maarufu wa pombe haramu aina ya gongo ,Abdulrazak Ismail, akilazika kuhama katika kijiji hicho baada ya jamii kukosa imani naye wakidai amekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa maadili.

Akizungumza baada ya msako huo Mwenyekiti wa Polisi jamii aliwataja vijana waliokamatwa kuwa ni Abdulrazak Ismail, pamoja na Said Mohammed.

Aidha alisema mbali ya kuwasaka watengenezaji na watumiaji wa pombe haramu aina ya gongo, pia utasaidia kukudhibiti wahalifu kutoka maeneo mengine ambao wamekuwa wakikimbia katika kijiji hicho baada ya kufanya uhalifu katika maeneo yao.