NA TATU MAKAME

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheri, ameutaka uongozi wa skuli ya Bumbwini Misufini kuutunza ukumbi wa mitihani ili utumike kwa muda mrefu.

Waziri Kheri alisema hayo Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Hassan Ali Kombo, wakati akizungumza na wananchi na uongozi wa skuli ya Bumbwini Misufini mara baada ya halmashauri hiyo kukabidhi ukumbi wa mitihani kwa skuli hiyo.

Alisema kazi iliyofanywa na halmashauri ya kujenga ukumbi wa mitihani kwa skuli hiyo ni mfano wa kuigwa na halmashauri nyengine za Zanzibar kutokana na umuhimu wake katika eneo hilo.

Aliutaka uongozi wa skuli kushirikiana na wananchi kuutumia kwa manufaa yaliyokusudiwa, na kuhakikisha wanautunza ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa.

Waziri Kheri, aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kuvifikia vianzio vyote vya mapato vilivyomo wilayani humo katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika suala zima la kuongeza mapato ikiwemo kulipa mkodi.

Aidha aliwataka watendaji kubuni vyanzo vipya vya mapato kwani ndio njia itakayoweza kufanikisha maendeleo mengine ikiwemo kutekeleza miradi ya maendeleo.