LONDON,UINGEREZA

WAZIRI  wa Mambo ya Ndani wa Uingereza amesema wakimbizi  wanaingia Uingereza wakitokea Ufaransa wakisema Ufaransa ni nchi ya kibaguzi.

Priti Patel aliliambia Bunge la Uingereza kwamba,wakimbizi wanaingia nchini wakisema Ufaransa ni nchi ya kibaguzi na kwamba mtazamo huo si wake yeye bali wa wakimbizi. 

Waziri wa Mambo ya ndani wa Uingereza alisema hayo baada ya kuongezeka idadi ya watu wanaohama Ufaransa na kuelekea Uingereza kwa kutumia mitumbwi.

Hadi sasa Ufaransa haijatoa tamko lolote kuhusu kadhia hiyo.

Wizara ya Mambo ya ndani ya Uingereza ilitangaza kuwa,Waziri Priti Patel alikasirishwa na idadi kubwa na inayoongezeka kila siku ya wakimbizi wanaotoka Ufarasa na kuingia nchini humo.

Maofisa wa Serikali ya Uingereza wamekuwa wakilalamikia idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia nchini humo kinyume cha sheria wakitokea Ufaransa kupitia mfereji wa English Channel.

Wanaharakati wa kutetea haki za wakimbizi pia wanalalamikia mienendo mibaya inayowakabili wakimbizi katika nchi za Ulaya ikiwemo Ufaransa na Uingereza.