BEIRUT, LEBANON

WAZIRI  wa mambo ya nje wa Lebanon ametangaza kujiuzulu kwake jana akiituhumu Serikali kuushughulikia vibaya mzozo wa kiuchumi uliowahi  kulikumba taifa hilo kwa miongo kadhaa.

Mzozo huo uliipelekea Serikali ya Lebanon kuomba msaada kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani IMF.

Waziri huyo, Nassif Hitti alisema Serikali ya Lebanon imeshindwa kutekeleza mabadiliko yanayotakikana na wafadhili wa kimataifa.

Mzozo huo wa kiuchumi ambao ni mbaya zaidi tangu  vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kati ya mwaka 1975-1990 ulisababisha mfumko wa bei kuongezaka na bei za bidhaa kupanda jambo linalosababisha umasikini, na maandamano ya raia wenye ghadhabu.

Serikali ya Waziri Mkuu Hasan Diab iliyoundwa mwezi Januari ilisemekana kuwa ni ya wataalamu ila imeshindwa kupata uungwaji mkono kimataifa.