NA MAULID YUSSUF, WEMA

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imesaini hati ya kukabidhiwa majengo ya maabara za sayansi ziliopo wilaya ya Wete baada ya kuridhishwa na matengenezo madogo waliyoyatoa hivi karibuni.

Utiaji saini wa hati hiyo umefanywa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk. Idrissa Muslim Hija na msimamizi wa ujenzi, mshauri elekezi Isack Peter Kika na meneja wa mradi huo kutoka kampuni ya Home Africa, Shukuru Yassin Kavenuke.

Akizungumza katika hafla hiyo huko Kojani, Dk. Idrissa alisema mwezi mmoja uliopita walifika kwa ajili ya makabidhiano ya majengo hayo, lakini kutokana na kutomalizika katika kiwango walichokubaliana hawakuyapokea.

Alisema walikataa kuyapokea majengo hayo na kuwaagiza wafanye marekebisho na kwamba marekebisho hayo yamefanywa hivyo wameyapokea.

Katibu huyo aliwashukuru na kumpongeza mkandarasi wa ujenzi huo kutokana na uvumilivu waliouonesha pamoja na kuwepo sintofahamu kati yao na wizara ambazo zilikuwa na lengo la kuimarisha ujenzi huo.

Dk. Idrissa alisema wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itaendelea kutoa mashirikiano na wakandarasi wa majengo yote katika miradi yao mbalimbali inayoianzisha kwa lengo la kupatikana mafanikio kwenye sekta hiyo.

Aliwataka wazazi na wananchi wa wilaya ya Wete kuhakikisha wanashirikiana katika kuyalinda na kuyatunza majengo hayo ili yaweze kudumu kwa faida yao na vizazi vijavyo.

Awali Naibu Katibu Mkuu Utawala na Uendeshaji, Abdullah Mzee Abdullah alisema ujenzi wa maabara hizo ni kutimiza ahadi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ya kutoa elimu bure.

Alisema utoaji wa elimu lazima uambatane kuwa na majengo ya kisasa yenye miundombinu rafiki kufundishia wanafunzi.

Alisema ili nchi iendelee kuzalisha wataalamu wazalendo ipo haja ya kuendelea kuimarisha elimu hasa masomo ya sayansi kwa kujenga maabara sehemu mbalimbali.

Naye  mkuu wa wilaya ya Wete, Mohamed Mussa Seif aliishukuru wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na kumpongeza Dk. Shein kwa uwamuzi waliouchukua  kuhakikisha maendeleo  ya elimu yanapatikana kwa wote.

Maabara tatu za sayansi zilizojengwa na kampuni ya Home Afrika zilizopo Fundo, Kojani na Limbani zimekabidhiwa kwa wizara ya Elimu kati ya maabara 22 zinazojengwa Unguja na Pemba kupitia mradi wa ZISP.