NA MAULID YUSSUF, WEMA

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imekabidhiwa ‘notes’ maalum na Jumuiya ya Madrasa Early Child hood, kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum ili ziweze kuwasaidia wakati wanapojiandaa na mitihani yao.

Akipokea ‘notes’ hizo huko ofisini kwake Mazizini mjini Unguja, Katibu Mkuu Dk. Idrissa Muslim Hija ameishukuru Jumuiya hiyo kwa juhudi kubwa inayochukua katika kuchangia maendeleo ya sekta ya Elimu nchini.

Alisema jumuiya ya madrasa Early Child Hood ni miongoni mwa taasisi zinazosaidia sekta ya elimu kwa kutoa ushauri juu ya masuala ya utungaji wa mtaala pamoja na namna ya kuzingatia majengo ya watu wenye mahitaji maalum.

Mapema akikabidhi ‘notes’ hizo, Mkurugenzi wa Madrasa Early child hood Khamis Abdalla Said alisema lengo la kuandaa ‘notes’ hizo ni kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum kusoma na kuweza kufanya mitihani yao bila ya matatizo.

Alisema ‘notes’ hizo wameziandaa maalum tangu wakati wa janga la maradhi ya corona ili ziwasaidie zaidi wanafunzi wa vijijini ambao kuna ugumu wa kusoma kupitia televisheni na redio.

Alisema ‘notes’ ni kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la 4, la sita na kidatu cha pili, ambapo pia wamewalipia wakalimani wa vipindi vya masomo ya televisheni kwa madarasa hayo ili wanafunzi wenye mahitaji maalum waweze kusoma wanapokuwa nyumbani kama Wanafunzi wengine.

Aidha aliishukuru wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa ushirikiano wanaowapatia ikiwemo kuandaa vipindi pamoja na ‘notes’ hizo kwa lengo la kuwasaidia watoto kusoma katika televisheni na radio.

Jumla ya kopi 244 za ‘notes’ za masomo zimetolewa na jumuiya ya madrasa Early child hood kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum chini ya ufadhili wa Jumuiya inayoshughulikia maendeleo ya watu wenye mahitaji maalum (NAD) kutoka Norway.