GENEVA, USWISS

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Afya Duniani amesema kuwa, kuna matumaini ya kudhibitiwa kikamilifu na kumalizika maambukizo ya kirusi cha corona kote ulimwenguni.

Shirika la habari la Reuters limemnukuu Tedros Adhanom akisema hayo jana na kusisitiza kuwa, kuna matumaini maambukizo ya kirusi cha corona yakamalizika katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Alisema, hata homa ya mafua ya Uhispania iliyojulikana kwa jina la Influenza ya Uhispania iliyotokea karne iliyopita na kuenea takriban mwaka 1918, nayo ilimalizika katika kipindi cha miaka miwili.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO aliongeza, kirusi cha corona kinaenea sana kutokana na maingiliano ya watu na inakuwa vigumu kukidhibiti madhali wanadamu hawajabadilisha tabia zao za kutofuata maelekezo ya watu wa afya.

Hadi kufikia jana asubuhi idadi ya watu waliokuwa wamethibitisha kuambukizwa kirusi cha corona duniani walikuwa wameshafikia 23,121,145. Waliokuwa wamepoteza maisha kwa ugoinjwa huo wa COVID-19 hadi leo asubuhi walikuwa ni 803,223 na waliopona walikuwa ni 15,715,254.

Marekani ndiyo inayoendelea kushika nafasi ya kwanza duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya maambukizi na vifo vya corona. Hadi leo asubuhi, Wamarekani 5,796,727 walikuwa wameshathibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo na 179,200 walikuwa wameshafariki dunia. 

Kwa upande wa barani Ulaya, Uingereza imeendelea kushika nafasi ya kwanza barani humo kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu waliofariki dunia kutoka na corona. Hadi leo asubuhi, Waingereza 41,405 walikuwa wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo hatari.