BEIJING,CHINA

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limetangaza kuwa limekamilisha uchunguzi wake nchini China kuhusu chanzo cha virusi vya corona.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom alisema kuwa, timu ya shirika hilo iliyokuwa safarini nchini China ilikamilisha kazi yake ya kutayarisha mazingira ya juhudi za pamoja za kutafuta chanzo cha virusi vya corona.

Adhanom aliongeza kuwa,shirika hilo pia litaanzisha utafiti wa kiepidemiologia katika mji wa Wuhan nchini China ili kubaini chanzo cha maambukizi ya virusi hivyo.

WHO ilisema kuwa kubaini chanzo cha virusi vya corona kutasaidia sana mapambano dhidi ya COVID-19 na kuitayarisha dunia kwa ajili ya kupambana na maradhi mengine ya baadaye ya kuambukiza. 

China ilikaribisha uchunguzi wa timu hiyo ya WHO ulioanza mwezi uliopita wa Julai lakini ilisisitiza kuwa, uchunguzi kuhusu chanzo cha virusi vya corona haupasi kuishia kwenye mipaka ya nchi hiyo.

Wiki kadhaa zilizopita China iliashiria matokeo ya baadhi ya tafiti zilizofanywa na wataalamu na kutoa wito wa kutiliwa maanani nchi ya Uhispania kama mojawapo ya nchi zilizokuwa chanzo cha mripuko wa virusi vya corona. 

Awali kuliripotiwa kuwa kuna ushahidi unaoonyesha kwamba, virusi vya corona vilikuweko nchini Uhispania miezi kadhaa kabla ya kuripotiwa kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi hivyo nchini China.