Waliokosa elimu, kukimbia skuli watakiwa kujiunga na madarasa ya mbadala

NA ABDU VUAI – IWMWW

KUFUATIA kuibuka kwa janga la corona mambo mengi yametatizika ambapo sekta ya elimu nayo ni miongoni mwa iliyofikwa na changamoto ya corona.

Kwa kuwa dunia inaadhimisha juma la elimu ya watu wazima kuanzia wiki hii tutaangalia namna ya elimu ya watu wazima ilivyowafikia walengwa hapa Zanzibar.

Elimu ya Watu Wazima imetoa mchango mkubwa wa maendeleo ya wananchi mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na hii ndio iliyokuwa miongoni mwa mikakati ya uongozi wa Rais wa kwanza Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume katika kupigana na maadui watatu ujinga, umasikini na maradhi.

Asilimia kubwa elimu ya watu wazima imewakomboa kimaisha kwa kutumia taaluma wanayoipata kupitia fani mbalimbali zinazotolewa chini ya usimamizi wa Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima.

Kupitia Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima serikali imetoa huduma ya Elimu kwa ajili ya wananchi wote wakiwemo watoto, vijana na watu wazima kwa kuwapatia fursa za elimu na ujuzi kupitia program wanazoziendesha ikiwemo kisomo cha watu wazima, Elimu Mbadala, Elimu ya Kujiendeleza, programu ya Wanawake, Sayansi Kimu nakadhalika.

Kutokana na umuhimu mkubwa uliopo katika program hii ya kisomo cha watu wazima, viongozi wa taasisi mbalimbali za elimu kutoka mataifa mengi ulimwenguni walikutana katika mkutano uliofanyika mwaka 1965 huko Tehran, na waliazimia kuwepo kwa siku hii ya kimataifa ya kisomo cha watu wazima yaani International Literacy Day (ILD) ambayo itakuwa tarehe 8 Septemba ya kila mwaka.

Mwaka 1966 ilitangazwa rasmi na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO, inayolenga kuibua hamasa kwa jamii kutokana na tatizo la kutojua kusoma ambalo linaendelea kuwepo katika jamii kitaifa na kimataifa.

Pia siku hii inakumbusha jamii ya kimataifa kufahamu umuhimu wa kisomo ndicho kitakachoiweka jamii kuishi kwa kuzngatia utu, maadili na haki za binadamu.

Nini kisomo, kwa mujibu wa kamusi la Miriam-Webster linaeleza kuwa kisomo ni hali kuweza kusoma na kuandika hasa kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii na hata mtu mmoja mmoja.

Shirika la UNESCO limetoa sababu tano zinazobainisha umuhimu wa kisomo kwa mtu ambazo ni Kuimarisha ubongo, ni kwamba kusoma, kuandika na kuhifadhi nambari kunaimarisha seli kwa kadiri msomaji anapozeeka pia hupunguza wasiwasi na mfadhaiko katika maisha yake.

Kupata fursa ya Kushiriki kijamii, hii humpa fursa mtu ya kupata kutoa michango mbalimbali katika jamii.  Kuweza kuwa na mawasiliano mazuri kwa kutumia njia tofauti za mawasiliano ikiwemo kuandika, kusoma na kutoa maoni na fikra kwa wengine. 

Vilevile kupata ajira, hupata kutumia fursa za ajira na kukuza uchumi kwani kisomo huvunja dimbwi la umasikini.

Na mwisho ni kuwa na nguvu, kwani kisomo ni ufunguo wa kumuwezesha na kumpa heshima mtu anaesoma.

Ujumbe wa maadhimisho ya siku ya Kisomo duniani kwa mwaka huu 2020 yatalenga katika “Ufundishaji na ujifunzaji wa kisomo chenye manufaa” unaolenga kukabiliana na Maambukizi ya janga la Covid – 19.

Sambamba na hilo kauli mbiu hii inalenga wajibu wa walimu wa kisomo katika kutumia mbinu bora ya ufundishaji.

Aidha, mwaka huu wa 2020 Wiki ya Elimu ya Watu Wazima itatoa fursa ya kuangazia upya na kuibua majadiliano juu ya namna ya ubunifu wa ufundishaji na mbinu muafaka za kufundishia kwa vijana na watu wazima ili kuweza kukabiliana na janga hili la corona.

Hapa Zanzibar mwaka huu 2020, maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima yataanzia na shamrashamra za michezo ambayo itanza keshokutwa Agosti 31 kutakuwa na mechi ya mpira wa miguu itakayowakutanisha timu ya Idara ya Elimu Mbadala na watu wazima na wanafunzi wa vituo vya kujiendeleza, mechi itakayochezwa katika uwanja wa Mao majira ya asubuhi.

Aidha maadhimisho yataendelea siku ya pili kwa kufanyika tathmini (mashindano) ya kusoma, kuandika na kufanya hesabu ndogondogo yatakayowashirikisha wanakisomo 100 wa hatua ya pili na ya nne kutoka wilaya ya Kaskazini ‘A’ na ‘B’, wialaya ya kisini na wilaya ya Magharibi ‘B’ shughuli ambayo itafanyika katika ukumbi wa kituo cha Elimu Mbadala Rahaleo.

Shamrashamra hizo zitaendelea siku ya Septemba 2 kwa kufanyika tathmini kama hiyo itakayowashirikisha wanakisomo takribani 60 wa hatua ya pili na ya tatu kutoka wilaya zote katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Madungu Pemba.

Kilele cha Wiki ya Elimu ya Watu Wazima mwaka huu 2020 kinatarajiwa kufanyika Septemba 3 kwa kufanyika kongamano katika ukumbi wa Makonyo, wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, ambapo atakagua shughuli mbalimbali za wanakisomo wa mikoa miwili ya Pemba.

Katika kongamano la wiki ya Elimu ya Watu Wazima jumla ya mada mbili zitawasilishwa na kujadiliwa na wataalamu na waliobobea katika bahari ya elimu hiyo isiyo rasmi pamoja na kutafuta mustakbali mzuri wa mandeleo ya elimu hapa nchini.

Mada zitakazojadiliwa katika kongamano hilo ni Tathmini ya hali ya kisomo Zanzibar ni pamoja na Miaka 10 ya Dk. Ali Mohamed Shein’, Kisomo chenye manufaa sambamba na mbinu bora za ufundishaji na ujifunzaji zitakazolenga kukabiliana na janga la maambukizo ya ugonjwa wa corona.

Hivyo idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima inawataka washiriki kuhakikisha kuwa wanahudhuria ili kujua kitakachoelezwa kwa faida yao.

Kutokana na umuhimu wa sekta ya elimu hapa nchini, taasisi na mashirika mbalimbali ya kiserikali na binafsi wamejitokeza kutoa michango yao ili kufanikisha maadhimisho hayo.