NA HUSNA MOHAMMED

WAKATI ulimwengu ukiadhimisha wiki ya kimataifa ya unyonyeshaji watoto na kuelezea faida zake kwa wazazi na taifa, wanaadamu duniani kote wanahamashishwa kufahamu umuhimu wa maziwa ya mwanzo kabisa ya mama kwa mtoto.

Takriban asilimia 40 tu ya watoto wachanga wenye umri kati ya miezi 0 hadi 6 ndio wanaoishi kwa kunyonyeshwa pekee, kulingana na shirika la Shirika la Afya duniani (WHO).

Kadhalika shirika hilo linasema kuwa zaidi ya maisha ya watoto 820, 000 walio na umri wa chini ya miaka mitano yanaweza kunusurika kila mwaka, ikiwa watoto wenye umri kati ya miezi 0 hadi 23 wangenyonyeshwa kikamilifu.

Wiki ya kimataifa ya kunyonyesha inaadhimishwa huku serikali za nchi mbalimbali wakitolewa wito kuwasaidia wanawake kuwanyonyesha watoto katika kipindi cha saa moja ya kwanza ya uhai wake.

Wataalam wanasema mguso wa mwili kwa mwili pamoja na kunyonya husaidia kuchochea uzalishaji wa maziwa ya mama, yakiwemo maziwa ya mwanzo kabisa ya mama baada ya kujifungua ambayo hutambuliwa kama”chanjo ya kwanza” , yenye virutubisho vingi pamoja na kinga ya ya mwili.

Kwa mfano hapa Zanzibar wataalamu wanasema ni asilimia 61 tu ya watoto wenye umri kati ya miaka 0-23 wanaonyonyeshwa katika muda wa nusu saa baada ya kuzaliwa na Mkoa wa Kusini Pemba upo nyuma zaidi ukiwa na asilimia 52.

Iwapo watoto wakicheleweshwa kunyonyeshwa kwa masaa 2 hadi 23 baada ya kuzaliwa inaongeza hatari ya kufa katika siku 28 za kwanza za maisha ya mtoto kwa asilimia 40.

Kitaalamu unyonyeshaji wa watoto hutakiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila kupewa chakula chengine kwa vile yanamsaidia kukua vizuri kiakili na kimwili.