Fahamu umuhimu wa unyonyeshaji wa ziwa la mama
Huleta faida kubwa kwa mtoto, mama, baba na taifa
NA MWANDISHI WETU
IKIWA dunia iko katika wiki ya unyonyeshaji inayoanza tarehe 1- 7 gazeti hili limeona iko haja kubwa ya kutayarisha makala inayoeleza umuhimu wa maziwa ya mama, au unyonyeshaji na faida zake kwa mama, baba, mtoto na Taifa kwa jumla.
Hii ni kusema kutokana na utandawazi kuna baadhi ya akina mama huwa hawawanyonyeshi watoto wao ipasavyo hasa hawa miongoni mwa umri wa miaka 20 mpaka 35 wakiwa na hofu kuwa maziwa yao yataanguka na kupoteza haiba yao katika jamii au labda watakataliwa na wenza wao.
UMUHIMU WA KUNYONYESHA MTOTO KWA MAMA
Jambo hili linasikitisha sana kwani kunyonyesha ni njia mojawapo muhimu inayomuunganisha mama na mtoto, sasa kama mtoto hatanyonya, hata ule ukaribu na mama pia hautakuwepo.
Kunyonyesha ni kitendo cha mama mzazi kumpa mtoto maziwa kutoka katika matiti yake moja kwa moja au kumnywesha mtoto maziwa ya mama yaliyokamuliwa kwa kutumia kikombe.

Maziwa ya mama ni chakula na kinywaji cha kwanza na cha pekee kwa mtoto mara tu anapozaliwa mpaka kufikia umri wa miezi sita bila kumpa hata maji ya kunywa.
Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) yanapendekeza mtoto aanze kunyonya maziwa ya mama saa moja baada ya kuzaliwa.
Maziwa ya mama ndiyo chakula bora kwa mtoto mchanga kuliko maziwa mengine yoyote yale au chakula kingine chochote. Maziwa ya mama ni chakula halisi cha kwanza kwa watoto, na yanawapatia watoto virutubisho vyote vinavyohitajika katika miezi ya mwanzo ya maisha yao.
Mtoto afikishapo umri wa miezi sita apewe vyakula vingine laini vya nyongeza huku akiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi kufikia miaka miwili au zaidi na hayo yako kwenye msisitizo wa kitabu kitakatifu cha Quraani kinachosoma mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo.
Kunyonyesha ni njia moja sahihi ya kuhakikisha mtoto anakuwa mwenye afya nzuri na kuendelea kuishi katika hali ya afya.
Kwa maana hiyo ziko faida nyingi sana anazopata mtoto, mama na baba kwa jumla.
FAIDA KWA MTOTO
Kumnyonyesha mtoto mara anapozaliwa kwa kipindi cha saa moja, humkinga kwa maambukizi yanayowapata watoto wachanga na kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Virutubisho vinavyopatikana kwenye maziwa ya mama, mchanganyiko wake ni wa kimaumbile zaidi. Kwa kuwa yanayotolewa kiasili, hayana gharama yoyote na ni salama zaidi. Yanaletea manufaa ya kisaikolojia vilevile, yanasaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya mama na mtoto mchanga.
Humpatia vyakula vyote sita vinavyojenga mwili (virutubisho) vyote anavyohitaji kwa uwiano ulio sahihi kwa ukuaji na maendeleo yake kama vile protein, vitamin, uwanga, sukari, maji na madini.
Unyonyeshaji bora wa maziwa ya mama hujenga uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto Humpatia kinga dhidi ya maradhi mbalimbali kama kuharisha, magonjwa ya njia ya hewa na masikio.
Maziwa ya mama humwezesha mtoto kukua kimwili na kiakili kiukamilifu.
Maziwa ya mama huleta uhusiano mzuri na wa karibu kati ya mama na mtoto.
Mtoto alienyonya maziwa ya mama huwa na mwenendo mzuri pamoja na akili ukilinganisha na yule asionyonya maziwa ya mama.
Kunyonyesha mtoto kunasaidia kumkinga mtoto na magonjwa mbalimbali yakuambukiza na yasioyakuambukiza.
Maziwa ya mama humweka mtoto salama na mwenye joto la kutosha akiwa pembeni mwa mama yake.
Unyonyeshaji wa mtoto humsaidia kuboresha uwezo wa utambuzi wa akili (IQ), mahudhurio ya skuli na pia huhusishwa na mapato ya juu katika maisha yake ya utu uzima.
Maziwa ya mama ni kinga inayodumu muda mrefu dhidi ya ugonjwa wa kisukari, mzio na saratani mbalimbali katika maisha ya mtoto ya baadaye.
FAIDA KWA MAMA

Maziwa ya mama huchangia katika kulinda afya yake kwa njia mbalimbali kama zifuatazo:
Mama anaponyonyesha mara baada ya kujifungua husaidia tumbo la uzazi kurudi katika hali ya kawaida mapema, ambapo husaidia kupunguza damu kutoka hivyo kuzuia upungufu wa damu.
Maziwa ya mama hupunguza uwezekano wa kupata ujauzito katika miezi sita ya mwanzo kama mama atamnyonyesha mtoto maziwa yake tu mara nyingi kwa siku na pia kama hajapata hedhi.
Hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya mfuko wa uzazi na matiti sambamba na kujenga uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto kwa unyonyeshaji bora wa maziwa ya mama.
Aidha iwapo mama aliongezekaa uzito mwingi wakati wa mimba, kunyonyesha husaidia kumrudishia mama umbile lake la kawaida.
Mama anapomnyonyesha mtoto wake hujengeka kiafya na kisaikolojia na mapenzi ya hali ya juu.
FAIDA KWA BABA
Maziwa ya mama gharama yake ni nafuu.hakuna haja ya kununua vyakula mbadala, chupa, au chochote kingine kwa hiyo baba hatotumia rasilimali yake.
Kwa vile maziwa ya mama ni kinga tosha kwa mtoto itampunguzia baba kutumia fedha kwa ajili ya matibabu ya mtoto.
Baba atapata muda wa kutosha wa kuhudumia watoto wenginge katika huduma muhimu na chakula, matumizi ya skuli na mavazi kwa jumla.
FAIDA KWA TAIFA
Ikiwa watoto watanyonyeshwa vizuri kutakuwa na punguzo kubwa la gharama ya matibabu hasa kwa wale wenye chini ya umri wa miaka 5 kwani watakuwa wamejengekeka vyema afya zao dhidi ya maradhi ya kuambukiza na yasiyo ambukiza.
INDHARI
Mtoto afikishapo umri wa miezi sita aanzishwe chakula cha nyongeza huku akiendelea kunyonya maziwa ya mama yake kwa mpangilio nzuri.
Baada ya miezi sita mtoto apewe chakula cha nyongeza kwa kutumia kikombe/ kibakuli na kijiko, tafadhali epukana na matumizi ya chupa.
Vyakula vya nyongeza viwe ni vya mchanganyiko wa makundi yafuatayo ya vyakula: – Vyakula vya nafaka, mizizi na aina za ndizi – Vyakula vyenye asili ya nyama – Mboga mboga na matunda – Mafuta na sukari kwa kiasi kidogo sana.
Mtoto aendelee kunyonya mpaka afikie umri wa miaka miwili au zaidi
Unyonyeshaji bora wa ni wa maziwa ya mama ndio njia pekee ya kumpa chakula na kinywaji mtoto wako, inawezekana timiza wajibu.