Uchaguzi usiwavuruge, endelezeni uzalendo

NA MADINA ISSA

MKUU wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Abeid Juma Ali, amewataka vijana kutojiingiza katika vurugu katika kipindi kinachoelekea  Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na badala yake kuendeleza uzalendo waliokuwa nao, ili taifa liendelee kuwa la amani.

Akizungumza na vijana huko Kianga, katika tamasha liloandaliwa na Baraza la Vijana wa Magharibi ‘A’ ikiwa ni sehemu ya wiki ya vijana dunia inayofanyika kila ifikapo Agosti 12 ya kila mwaka.

Alisema vijana hawana budi kuendeleza uzalendo na kuipenda nchi yao sambamba na kudumisha umoja na mshikamano na mahusiano mazuri kwa vijana wenzao itapeleka amani kudumu katika taifa.

Alisema, kuundwa kwa mabaraza ya vijana inapeleka kuwaunganisha vijana wa Zanzibar katika Nyanja tofauti za kijamii na kiuchumi pamoja na kuwajengea uzalendo wa kuipenda nchi.

Aidha alisema kuwa serikali ya wilaya imekuwa ikithamini jitihada za vijana wanazozifanya ikiwemo kutoa elimu kwa vijana wenzao, ili kuona wanakuwa katika msitari wa kuendeleza amani ya nchi.

“Sisi serikali tupo na nyinyi bega kwa bega kwa kuona changamoto zenu zinatatulika kwa wakati, kwani mumekuwa mstari wa mbele kutusaidia kuwahamasisha vijana wasijiunge katika makundi maovu” alisema.