NA MWANDISHI WETU

IKIWA waislamu kote ulimwenguni wako katika shamrashamra ya kuusherehekea mwaka mpya wa kiislamu 1442, ni vyema kwa muislamu ajue lini mwaka huu ulianza na kwa nini uliitwa mwaka wa hijra.

Kabla ya hijra (Mtume kuhama kutoka Makka kwenda Madina) waislamu walikua wakijua tarekhe zao kupitia kuzaliwa kwa Mtume mfano, Sayyidina Uthman alizaliwa mwaka wa 6 baada ya kuzaliwa Mtume baada ya mMume kupewa utume wakaanza kuhesabu tarekhe kwa kutimilizwa kwake ambapo Sayyidina Omar alisilimu mwaka wa 5 baada ya Mtume kutimilizwa. 

Na kabla ya hapo walikuwa wakizijua tarekhe kwa kutumia mwaka wa miladia yaani tangu kuzaliwa Nabii Issa (A.S), Nabii Mohammad alizaliwa mwaka 571M tangu kuzaliwa Nabii Issa (A.S).

Ama miezi hii ya muandamo muhrram mpaka dhul hijja, hii ilikuwepo toka Mwenyezi Mungu alipoumba mbingu na ardhi na  idadi yake kama Qur’an inavyotueleza ni 12 (qur’an 9:36).

Ila tu haikujulikana kama sasa tuko mwaka wa ngapi na ndiyo maana ikajulika tu kihistoria kwamba Mtume alizaliwa mwezi wa Rabi’unil aw wal (mfunguo sita) ambao ni mwezi wa tatu kwa utaratibu wa kalenda ya kiislamu kama tutakavyoona. 

Mwezi wa kwanza ni muhar ram, wa pili ni swafar  wa tatu ni Rabi’unil aw wal, wa nne ni Rabi’unith thaani, wa tano ni Jumaadal ulaa, wa sita ni Jumaadath thaania, wa saba ni Rajab, wa nane ni Sha’aban, wa tisa ni Ramadhani, wa kumi ni Shaw waal, wa kumi na moja ni Dhul qi’da, na wa kumi na mbili ni Dhul hujjah.

Mtume alizaliwa katika mji wa Makka tarekhe 12/3 (mfunguo sita) siku 50 baada ya tukio la kuangamizwa Abraha (al ashram) pamoja na Jeshi lake (watu wa tembo) ambao tangu kuzaliwa Nabii Issa (A.S) ulikuwa ni mwaka wa 571 miladia.

Aliishi Makka Mtume  ( baada ya kupewa utume akiwa na umri wa miaka 40) kwa muda wa miaka 13 kisha akaamrishwa kuhamia Yathrib ambayo baadaye na mpaka sasa inaitwa al madinatul munaw wara.

Baada ya kuhamia Madina Mtume aliishi  kwa muda wa miaka 10 kisha akafariki dunia ikiwa bado waislamu hawajawa na hesabu ya mwaka huu wa kiisilamu.

 Hivyo basi, ulipofika mwaka wa 17H katika khilafa ya Sayyidina Omar ndipo fikra za tarekhe zikaanza.