NA HAFSA GOLO

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema itaendelea kufatilia kwa karibu vituo vyote vya afya ili kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa maradhi ya mripuko ya kuharisha na kutapika katika kipindi hichi cha mvua zilizoanza kunyesha nchini.

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya Dk. Fadhil Mohamed, alieleza hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Vuga mjini Unguja.

Alisema zoezi hilo limekusudia kutambua kama wapo baadhi ya wagonjwa waliojitokeza  kuugua maradhi hayo, ili mikakati iendelee kutekelezwa ipasavyo.

Dk. Fadhil alisema, ufatiliaji huo pia utaangalia yale maeneo sugu ambayo yamekuwa ni  miongoni mwa chanzo cha kuibuka kwa maradhi ya kuharisha na kutapika nchini, ili hatua za kinga na tiba zichukuliwa mapema na kwa wakati stahiki.

“Tunawaomba wananchi kushirikiana na wataalamu wa afya na mtu yoyote atakaebaini dalili za ugonjwa huo aende katika kituo cha afya kilichokaribu naye badala ya kutumia dawa bila ya maelekezo ya wataalamu”,alisema.

Katika juhudi hizo alishauri viongozi wa Baraza la          Manispaa kuhakikisha wanasimamia kwa vitendo masharti na taratibu za uzaji wa biashara za vyakula kwani kufanya hivyo itamsaidia mlaji.

Aliwataka  wananchi kuchukua tahadhari kwa kufuata  miongozo inayotolewa na wataalamu wa afya, ikiwemo kuchemsha maji ya kunywa, kunawa mikono kwa maji ya vuguvugu sambamba na kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama.

Nae Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Mjini, Said Juma Ahmada alisema, tayari baraza hilo, linaendelea kufatilia kwa karibu na tayari wapo baadhi ya wafanyabiashara waliokiuka masharti na taratibu sheria imeshachukua mkondo wake. 

Aidha alisema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kutozwa faini na wengine kuzuiliwa kufanya biashara hadi watakapotimiza maelekezo yaliotolewa kuhusiana na usafi wa mazingira.